Na Calvi Gwabara – Mbarali.

 
Serikali Wilayani Mbarali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
pamoja na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa
jitihada zao za kusaidia kurejesha uoto wa asili kwenye vyanzo vya maji pamoja na kufanya utafiti na kutoa matokeo ambayo yataisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali Denis Mwila wakati akifungua warsha ya kutoa matokeo ya utafiti wa Mradi wa usimamizi endelevu wa madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na athari za shughuri za kibinadamu Tanzania (EFLOWS) iliyofanyika Wilayani humo Mkoani Mbeya.


“Kuna athari kubwa ya kiusalama ambayo inaonekana kuja kwa juu kwa sasa ya
uharibifu wa mazingira lakini ukiangalia kwa makini na kwa mujibu wa vitabu
kadhaa nilivyosoma inaonekana vita ya tatu ya dunia itakuwa ni vita ya maji na hii imeanza kudhihirika kwenye maeneo mbalimbali na mfano mzuri ni eneo la mto Nile na hata ninapopita kwenye wilaya yangu kuongea na Wananchi swala la maji ndio kilio kikubwa” alieleza Mhe. Kanali Mwela.


Aidha matokeo hayo mazuri ya kina na kisayansi ya utafiti ya Mradi wa
EFLOWS watayapitia vizuri na kuyatumia katika kutekeleza mipango mbalimbali ya uhifadhi kupitia mapendekezo yaliyotolewa ili kusaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na mazingira kwa manufaa mapana na Taifa kwa kuwa vyanzo vya maji vilivyo nyanda za juu kusini ndivyo vinavyotegemewa kutiririsha maji yake kwenye mto Ruaha mkuu na hatimae Bwawa la Kidatu na Mwl. Nyerere.


Amesema kuwa kumekuwa na uelewa kidogo wa jamii na baadhi ya viongozi
katika masuala ya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji ndio maana Serikali
inapochukua hatua za kuzuia shughuli fulani za kibinadamu kwenye maeneo
muhimu ya vyanzo vya maji na hifadhi huzuka malalamiko mengi ambayo chanzo chake kikubwa ni ubinafsi wa watu wachache usiojali maslahi ya watu wengi na Taifa.


“Nyanda za juu wasipotunza vyanzo vya maji na kufuata sheria za uhifadhi wa
mazingira Mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere
hautafanya kazi na hivyo kusababisha nchi kukosa umeme wa kutosha kuendesha Viwanda, Treni ya Mwendokasi (SGR) na shughuli zingine za jamii zitakwama maana nishati hii ni muhimu kwa kila mtu” alieleza Kanali Mwela.


Mhe. Kanali Mwela amepongeza kazi hiyo kubwa ya utafiti iliyofanywa na SUA
kwa kushirikiana na NEMC katika kufanya tathimini ya mtiririko wa maji kwenye
mto Mbarali ambao unachangia maji yake kwenye Mto Ruaha mkuu na hatimae
kuelekea Bwawa la Mwl. Nyerere na kwamba matokeo hayo yanasaidia kuonesha vizuri hali halisi ya vyanzo vya maji na mtiririko wake na nini kifanyike.


Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS kutoka (SUA) Prof. Japhet
Kashaigili amesema katika kipindi cha miaka miwili ya utafiti huo tathimini ya kina imefanyika kuangalia hali ya vyanzo vya maji vya mto Mbarali, Afya ya Mto, Maumbile ya mto na uoto wake kupitia wataalamu waliobobea nchini kwenye nyanja hizo kutoka taasisi mbalimbali nchini na wananchi wa maeneo hayo hususani Jumuiya za watumia maji.


“Wakati tunakuja kutambulisha mradi tuliitana wadau wote wa maji wa mto
Mbarali na tukawaeleza malengo ya ujio wetu wa utafiti huu na wengi wenu
mlishiriki pia wakati wa utafiti wenyewe katika kipindi chote na baada ya
kukamilisha kuchakata matokeo ya yale tuliyoyaona kisayansi sasa tumeona ni
vyema kurudi tena kwenu kuwapatia mrejesho ili kwa pamoja tujue tunawezaje
kutumia matokeo hayo kwa pamoja kusaidia kulinda vyanzo vya mito yetu na
mazingira kwa faida ya Taifa” alieleza Prof. Kashaigili.


Aliongeza kuwa“ lengo la pili ni kujadili hatua za kuchukua ili kufikia malengo ya
usimamizi na mpango wa utekelezaji na kuainisha wadau, majukumu, mpango na ushirikiano ili sote kwa pamoja tukubaliane cha kufanya na kushiriki kikamilifu
maana tunategemeana na tunakwenda na usemi uleule kuwa ukitaka kufika mbali nenda na wenzako ila ukitaka kwenda haraka nenda peke yako na sisi lengo ni kufika mbali hivyo lazima twende pamoja”.


Prof. Kashaigili amesema takwimu na sampuli zilikusanywa kwenye maeneo
manne waliyoyateua kupitia vigezo mbalimbali na zoezi hilo lilifanyika wakati wa
kiangazi wakati kina cha maji mtoni kiko chini na wakati wa masika kipindi mto
umejaa maji kuanzia mwanzo mwa mto katika eneo la Wilaya ya Wanging’ombe
na Mbarali ambako unaishia na kumwaga maji yake kwenye mto Ruaha mkuu.


Nae Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka (NEMC) Dkt. Menan
Jangu amesema Baraza linajukumu kubwa la kuhakikisha miradi mikubwa inayoanzishwa inafikia malengo kwa kupata mahitaji yanayohitajika kwa kupitia
utunzaji wa mzingira na vyanzo vya maji.


Amesema ni wazi kuwa Mazingira, Ikolojia, bioanuai na huduma zinazopatikana
zinaendelea kupata changamoto kubwa kutokana na ongezeko la watu, ongezeko la mahitaji na kwamba changamoto hizo zisipopatiwa ufumbuzi rasiliamali nyingi zinaweza kutoweka hususani mtiririko wa maji ambao ni uhai wa Wanyamapori, Binadamu na Miradi mikubwa ya uzalishaji wa nishati nchini.


“Utekelezaji wa utafiti huu ni moja ya malengo ya NEMC katika kuhakikisha
kunakuwepo na tafiti nzuri na za kina ambazo zinafanywa nchini katika eneo la
mazingira ili kupata matokeo na suluhu za kisayansi ambazo zitasaidia kuhifadhi
mazingira na vyanzo vya maji pamoja na mbinu za kurejesha uhalisia kwenye
meneo ambayo yameathiriwa na shughuli za kibinadamu au majanga ya asili”
alieleza Dkt. Jangu.


Hata hivyo amesema matokeo ya utafiti huo yanatoa muelekeo wa hali ilivyo na kujua kama ni bado ni muelekeo sahihi au kuna maeneo ya kufanyiwa kazi na ndio maana kwenye eneo la utafiti NEMC inafanya kazi na wadau pamoja na taasisi zingine kama ilivyo kwenye mradi huu kati ya SUA, NEMC na wadau wengine.


Mradi huu wa Utafiti unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutekelezwa katika bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa ushirikiano na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa
ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, kupitia michango
ya nchi kumi wanachama wa Azimio la Nairobi ambapo kwa Tanzania ni kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, katika kutekeleza Mpango Mkakati wa
Kivitendo wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi chini ya uratibu wa Sekretarieti ya
Azimio la Nairobi.


Dkt. Winfred Mbungu akitoa matokeo ya tathimini ya maji kwa mazingira na mtiririko wake kwenye mto Mbarali





Mbarali Disctrict Commissioner ,Hon.Col. Denis Mwila speking during the opening of the Workishop.

Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka (NEMC) Dkt. Menan Jangu akitoa salamu za NEMC.

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS kutoka (SUA) Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya warsha hiyo.

Picha ya pamoja baadhi washiriki wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...