Na Said Mwishehe, Michuzi TV
NCHI za Tanzania na Uganda zimeamua kuingia makubaliano ya ushirikiano katika udhibiti wa magonjwa ya wanyama yanayovuka mipaka na yanayoambukiza binadamu kutoka kwa wanyama katika maeneo ya mipakani.
Makubaliano ya ushirikiano huo yamefanyika leo Septemba 7, 2023 kati ya Waziri wa Mifugo, Abdalla Ulega na Waziri wa Mifugo wa Uganda , Bright Rwamirama wakati wa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika(AGRF) unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuingia makubaliano hayo Waziri Ulega ameeleza kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeathiriwa na magonjwa ya wanyama yanayovuka mipaka na yanayoambukiza binadamu kutoka kwa wanyama.
Amefafanua kuwa uwepo wa magonjwa hayo umeathiri uzalishaji na uzalianaji wa mifugo, afya ya jamii, usalama wa chakula , uhifadhi wa wanyamapori , utalii na biashara ya mifugo na mazao yake.
Ameongeza ni muhimu kuwepo kwa mkataba wa makubaliano utakaowezesha ushirikiano wa pamoja katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kudhibiti magonjwa yanayovuka mipaka na yanayoambukiza binadamu kutoka kwa wanyama.
Ametumia nafasi hiyo kutaja baadhi ya magonjwa yanayovuka mipaka ni homa ya mapafu ya ng'ombe,nguruwe mbuzi, sotoka ya mbuzi na kondoo, kideli, ugonjwa wa miguu, midomo na mapele ya ngozi.
Wakati kwa magonjwa yanayovuka mipaka na kuambukiza binadamu ni Ebola, Marburg, homa ya bonde la ufa, na homa nyingine zinazoambatana na damu kuvilia mwilini, mafua makali ya ndege na kimeta.
"Katika mpaka wa Tanzania na Uganda kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa mifugo, wanyamapori na mazao ya wanyama jambo ambalo limekuwa likihatarisha kusambaa kwa magonjwa ya wanyama kwa kila upande," ameeleza Waziri Ulega.
Akielezea zaidi maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizo ni kufanya utaratibu, utambuzi na udhibiti wa wanyama , kuendeleza miundombinu ya mifugo iliyopo mipakani na rasilimali watu na kitumia teknolojia za kisasa.
Pia kuna mipango ya pamoja ya utafiti na udhibiti wa magonjwa hayo na maeneo mengine kulingana kama yatakavyokubaliwa na kamati ya pamoja na wataalamu.
Pamoja na hayo amewataka wakurugenzi wa mifugo wa nchi za Tanzania na Uganda wahakikishe wanachukua hatua na kalenda zao ziwe zinawiana katika uchanjaji.
Kwa upande wakeWaziri wa Mifugo wa Uganda Bright Rwamirama baada ya kuingia makubaliano ya ushirikiano huo amesema makubaliano hayo yataleta tija kwa pande zote mbili.
Amesisitiza kupitia ushirikiano huo sekta ya mifugo watahakikisha inakuwa na tija kwa wafugaji wa nchi hizo katika harakati za kukuza uchumi.
Ameongeza kwamba silimia 70 ya magonjwa ya binadamu yanatokana na mifugo hivyo lazima kuwepo na mikakati madhubuti ya kuhakikisha magonjwa hayo yanadhibitiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...