-Waziri Mkumbo ataja mabilioni ya fedha yatakayoingia kila mwaka, Ajira 100, 000
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ameelezea manufaa makubwa ambayo nchi ya Tanzania itapata kutokana na ujenzi wa eneo la Uwekezaji wa Sinotan Industrial Park katika eneo la Kibaha mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo ni kwamba ujenzi wa viwanda takribani 200 vitakavyojengwa eneo utakapokamilika Tanzania itakuwa inapata Sh.trilioni moja kwa mwaka katika eneo hilo la uwekezaji na takriban ajira 100, 000 za muda mfupi na mrefu zitapatikana .
Profesa Mkumbo ameeleza hayo leo Septemba 25, 2023 akiwa katika eneo hilo la Sinotan Industrial Park wakati wa ziara ya wawekezaji kutoka nchini China zaidi ya 120 kutembelea eneo hilo ambapo miongoni mwao wameonesha nia ya kujenga viwanda vikiwemo vya nguo, viatu na dawa.
Akielezea zaidi Profesa Mkumbo amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia hotuba yake aliyoitoa Aprili wakati anahutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka wazi maono yake katika kuvutia uwekezaji kwa kuwa na mazingira yanayovitia wawekezaji kuwekeza nchini.
"Leo hii hapa tukishudia mafanikio makubwa ya dira ya Rais Samia suluhu Hassan kutokana na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji , tunashuhudia uwekezaji wa zaidi ya Sh.bilioni 800.Hapa Tanzania kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia Industril Park.
"Tumekuwa tukizungumzia maeneo ya kujenga eneo la uwekezaji lakini hapa tulipo ndio unapata maana halisi tunaposema eneo la uwekezaji.Kutakuwa na viwanda 200 ambavyo vitajengwa hapa ndani vikiwemo viwanda vya msingi, " amesema Profesa Mkumbo.
Amesema kutokana na ujenzi wa viwanda hivyo vikiwemo vya nguo maana yake Pamba inayozalishwa nchini katika mikoa takribani 17 itapata soko la uhakika kwani kwa sasa asilimia 80 ya pamba inauzwa nje ya Tanzania.
Pia amesema kupitia eneo hilo la uwekezaji sekta ya mifugo nayo inakwenda kufungamanishwa na viwanda kwani kunatarajiwa kujengwa viwanda vya viatu, hivyo ngozi itapata soko la uhakika.
"Kutakuwa na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha dawa, pia kutakuwa na viwanda vya kutengeneza kemikali mbalimbali.Lakini eneo hili linakwenda kuwa mji mkubwa wa viwanda na ujenzi huo utakamilika mwaka 2025 , hivyo ajira zaidi ya 100, 000 zinakwenda kupatikana.
"Fedha ambazo zitakuwa zinapatikana hapa ni Sh.trilioni moja kwa mwaka.Nimpongeze Mwenyekiti wa Group Six Internatiaonal , Sinotan Industrial Park Janson Huang kwa kuhamasisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza katika eneo hili.
"Hawa wawekezaji wanaweza kumsikiliza Rais, Waziri, TIC lakini wanasikiliza zaidi wakimsikiliza mwenzao.Hivyo nikupongeze Janson Huang kwa kufanya kazi hii, ",amesema Profesa Mkumbo .
Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na China amesema ni wa zaidi ya miaka 60 huku akifafanua China imeisaidia katika ukombozi lakini wamesaidia katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli ya TAZARA wakati dunia nzima ikiwa imekataa.
"China wameamua kuwekeza katika viwanda, mnafahamu wiki iliyopita Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amezindua kiwanda cha kutengeneza vioo ambacho ni kikubwa katika Afrika Mashariki na leo tunazindua kiwanda kikubwa eneo hili la Sinotan.Niwaombe na kuwaalika wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza katika eneo hilo."
Kwa upande wake Naibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema maono ya Rais Dk.Samia ni kuona uwekezaji unawezekana na eneo hilo linadhihirisha mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji.
"Tutaendelea kuangalia namna gani ya kuboresha biashara na kama kuna changamoto zozote tutazitatua kwa haraka ili kuvutia uwekezaji, " amesema Kigahe.
Ameahidi Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na na Wizara ya Uwekezaji na TIC kuhakikisha wanaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyabiashara na uwekezaji.
Kuhusu uwekezaji katika eneo la Sinotan amesema wanatarajia kuona uwekezaji huo utakuwa na faida nyingi kwa Watanzania wote wakiwemo wa Kibaha mkoani Pwani.
Awali Mwenyekiti wa Bodi wa Kituo cga Uwekezaji Tanzania( TIC) Dk.Binilith Mahenge ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Kuhusu eneo la uwekezaji uliofanywa na Sinotan Industrial Park, Dk.Mahenge amesema eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya uwekezaji ni hekta 2500 na kiasi cha fedha cha fedha ambacho kimewekezwa ni Dola za Marekani milioni 327 huku Opereta wakitarajiwa kuweka zaidi ya dola za Marekani Bilioni tatu.
Aidha amesema katika eneo hilo awali eneo hilo lilikuwa na changamoto ya kuchelewa kuwepo kwa vivutio vya uwekezaji lakini Serikali kupitia TIC wamemaliza changamoto na tayari kuna vivutio.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Group Six Internatiaonal , Sinotan Industrial Park Janson Huang amefafanua kwa kina kuhusu uwekezaji unaoendelea kufanywa eneo hilo sambamba na wawekezaji kutoka China kuonesha kiu ya kujenga viwanda katika eneo la Sinotan.
Wawekezaji kutoka China wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali za Tanzania na China baada ya kufanya ziara eneo la uwekezaji la Sinotan Industrial Park lililopo Kwala wilayani Kibaha mkoani Pwani
Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo akiwa na Mwenyekiti wa Group Six Internatiaonal , Sinotan Industrial Park Janson Huang wakionesha michoro ya eneo hilo la uwekezaji
Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa ziara ya wawekezaji kutoka nchini China kutembelea eneo la Sinotan Industrial Park lililopo Kibaha mkoani Pwani
Matukio mbalimbali katika picha baada ya wawekezaji kutoka nchini China zaidi ya 120 kutembelea eneo la Sinotan Industrial Park kufanya ziara katika eneo hilo kuangalia fursa za uwekezaji
Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo( kulia) akipongezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dk.Binilith Mahenge( kushoto).Katikatika ni Naibu Waziri wa Viwanda Exaud Kigaye
Sehemu ya wawekezaji kutoka China wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo( hayupo pichani) baada ya kutembelea eneo la uwekezaji la Sinotan Industrial Park
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...