Benki ya Absa Tanzania imesema itaendelea kufanya uwekezaji mkubwa zaidi kupitia huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kufanya huduma za kibenki nchini kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu na hivyo kuwafikia watu wengi zaidi.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bwana Obedi Laiser wakati akizundua wiki ya huduma kwa wateja akisema kuwa wamejipanga katika kuhakikisha wateja wao wanapata huduma zenye viwango vya kimataifa wawapo katika matawi yao nchini kote ama wawapo nje ya matawi kwa kutumia huduma za kidigitali.
“Tunajivunia wateja wetu, ninyi ndio msingi na sababu ya sisi kuwepo, tumewaita ili tukae pamoja na kuwasikiliza ni namna gani mngependa tuwahudumie, lakini lililo kubwa zaidi ni kutumia muda huu kuwashukuru kwa msaada na ushirikiano wenu wa kibiashara.
“Kwa niaba yangu na timu nzima ya benki yetu tunaahidi kuendelea kuwahudumia vizuri kwa huduma bora na za kiubunifu zinazokidhi mahitaji yenu ya kibenki,” Bwana Laiser akawaambia baadhi ya wateja waliohudhuria hafla hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Lilian Swere alisema Absa imekuwa ikitoa huduma zake kwa kiwango cha juu sawasawa na maoni ya wateja kama ambavyo wamefanya katika mwaka huu kwa kuingiza bidhaa na huduma mbalimbali tofauti sokoni.
Akitaja baadhi ya huduma, Bi Ndabu alitaja huduma za mikopo hususani mikopo ya nyumba iliyoboresha ambapo sasa mteja anaweza kujenga ama kununua nyumba kutoka taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya nyumba walizoingia nazo makubaliano. “Kingine kilicho kizuri baada ya kusikia maombi ya wateja wetu tumeweza kurekebisha mikopo yetu isiyo na dhamana ambapo wateja wetu wanaweza kukopa hadi sh milioni 150 kwa masharti nafuu kabisa bila kusahau huduma yetu ya Absa Wakala tuliyoizindua hivi karibuni ambayo wateja wetu wanaendelea kufurahia ofa ya miezi miwili ya kufanya miamala kwa mawakala wetu bila ada,” alisema Bi. Ndabu.
Wiki ya huduma kwa mteja mwaka huu inakwenda kwa kauli mbiu isemayo ‘Team Service’ ikiwataka wafanyakazi wa kwa ujumla wao kuungana kwa pamoja katika kutoa huduma bora kwa mteja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Obedi Laiser (wa tatu kutoka kulia), akigonganisha glasi kupongezana na kutakiana mafanikio na baadhi ya wateja na wafanyakazi wa benki hiyo, wakati wa sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ya Absa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Obedi Laiser (kushoto), akishikana mikono na mteja wa benki, Bwana Simon Jengo, wakati wa sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ya Absa jijini Dar es Salaam leo. Katikati ni Mkuu Kitengo cha Biashara wa Absa, Bwana Melvin Saprapasen.
Mkuu wa Mikakati na Bidhaa Rejareja wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Heristraton Genesis (kulia), akisalimiana na mmoja wa wateja wa benki hiyo, Jaji Thomas Mihayo, wakati wa sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ya Absa jijini Dar es Salaam leo. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Obedi Laiser.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...