Na Mwandishi Wetu


Benki ya Exim imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Jeshi la Polisi la Tanzania unaolenga kuwezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa askari polisi kupitia program maalum ya benki hiyo ijulikanayo kama ‘Wafanyakazi Loan’.

Makubaliano hayo mapya yaliyotiwa saini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki yanadhihirisha azma ya benki ya Exim ya kuendelea kuwawezesha watanzania kifedha kupitia utoaji wa huduma za kibenki na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini kote.

Akizungumza kabla ya utiaji saini huo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Shani Kinswaga alieleza matumaini yake kuwa mkataba mpya uliotiwa saini kati ya benki yake na Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mahusiano baina ya taasisi hizo mbili.

Kinswaga alisema benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kukuza sekta ya kifedha kwa kutoa huduma za kifedha bila vikwazo, huku ikitumia suluhu za kidijitali na huduma zinazotengenezwa mahususi.

“Tumefanya vikao na Jeshi la Polisi kuhusu jinsi tunavyoweza kutekeleza azma yetu ya kutoa mikopo kwa askari wa Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika. Tunayo furaha leo kwa kuwa majadiliano yetu yametimia kwa kusaini mkataba huu. Kama benki, tunashukuru kwa fursa hii ya kipekee na imani tuliyopewa na tunaamini mikopo itakayotolewa kupitia program yetu ya ‘Wafanyakazi Loan’ itakuwa chachu ya maendeleo," Kinswaga alisema.

Alibainisha kuwa kupitia program hiyo maalum ya ‘Wafanyakazi Loan’, askari polisi wataweza kukopa kuanzia shilingi milioni moja hadi shilingi milioni 160 ambayo inaweza kurejeshwa kati ya miezi 6 hadi miezi 96 kutegemeana na ahadi ya mkopaji ambayo inaweza kutumika kutekeleza ndoto za mkopaji ikiwa ni pamoja kupata mkopo wa nyumba, kununua magari na kulipia ada ya masomo ili kuendeleza kieleimu.

“Tofauti na mikopo mingine iliyopo sokoni kwa sasa, wakopaji kupitia programu yetu ya ‘Wafanyakazi Loan’ hawalazimika kutoa dhamana yoyote kama sharti. Mkopaji anahitaji tu kuwa na hati ya mishahara, taarifa ya benki na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake na baada ya kukidhi mahitaji hayo machache, mkopaji atapokea mkopo yake ndani saa 48 tu,” Kinswaga alisema.

Hata hivyo alitoa angalizo kwa wakopaji kupitia programu hiyo kuhakikisha kutumia fedha zilizokopwa kwa busara kutekeleza miradi ambayo itaongeza thamani huku alkiwasihi kuandaa mpango maalum wa marejesho ili kuhakikisha kwamba mikopo hiyo inalipwa kwa wakati.

"Benki ya Exim, tuna shauku ya kutengeneza fursa kwa wateja wetu. Ni matumaini yangu kuwa endapo mikopo hii itatumika vyema, basi itasaidia kutoa suluhu mbadala za kifedha kwa maafisa wa polisi ili kutimiza ndoto zao,” aliongeza.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi, Fedha na Lojistiki, Liberati Sabas Materu aliyemwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camilius Wambura wakati wa hafla hiyo alisema makubaliano hayo yamekuja wakati muafaka na kuishukuru Benki ya Exim kwa imani yake kwa Jeshi la Polisi Tanzania.

“Wachumi wanaamini kuwa huwezi kufanya maendeleo bila kukopa lakini hili linahitaji nidhamu kubwa. Naishukuru Benki ya Exim kwa kuendelea kuwa na imani na taasisi yetu na kuridhia kutoa mikopo kwa maafisa wetu wa polisi na ninaamini mikopo hii itasaidia kuboresha ustawi wao wa kijamii na kiuchumi iwapo itatumika ipasavyo,” CP Materu alisema.

CP Materu wakati wa hafla hiyo alisisitiza dhamira ya Polisi Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Benki ya Exim ili kuhakikisha kuwa mpango huo wa ‘Wafanyakazi Loan’ unakuwa na tija kwa askari wa Jeshi la Polisi.

“Kama taasisi, tuna mifumo thabiti na tutahakikisha kwamba makubaliano haya yanatelezwa kwa ukamilifu. Yeyote atakayeweza kupata mkopo kupitia programu hii atakuwa na wajibu wa kulipa kama ilivyokubaliwa hapo awali,” aliongeza.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shan Kinswaga (wa pili kulia) na Kamishna wa Polisi, Liberati Sabas Materu (katikati) wakitia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki utaowezesha utoaji wa mikopo kwa askari wa Jeshi la Polisi Tanzania kupitia programu maalum ya ‘Wafanyakazi Loan’ ya Benki ya Exim. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Benki ya Exim Edmund Masaga, Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Jeshi la Polisi Tanzania ASP Ezekiel Midala (wa pili kulia) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Gustavus Babile (kulia).

Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shan Kinswaga (wa tatu kulia) na Kamishna wa Polisi, Liberati Sabas Materu (wa tatu kushoto) wakionyesha nyaraka mara baada ya kutiliana saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki utaowezesha utoaji wa mikopo kwa askari wa Jeshi la Polisi Tanzania kupitia programu maaluum ya ‘Wafanyakazi Loan’ ya Benki ya Exim. Wa pili kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Benki ya Exim Edmund Masaga, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Stanley Kafu (kulia), Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Jeshi la Polisi Tanzania ASP Ezekiel Midala (kushoto) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP). ) Gustavus Babile (wa pili kushoto).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...