NA WILLIUM PAUL, Moshi.
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro inatarajia kuanza ziara ya siku tisa kutembelea majimbo yote tisa ya mkoa wa Kilimanjaro ambapo inatarajia kufikia kata 63 na kufanya vikao vya ndani vya chama na badae mikutano ya hadhara ya wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alipozungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema kuwa, ziara hiyo inatarajiwa kuanzia katika Jimbo la Siha, likifuatiwa na Jimbo la Rombo, Mwanga, Moshi vijijini, Vunjo, Moshi mjini, Hai, Same mashariki na kumalizia na Same magharibi.
"Ili kuhakikisha tunafikia kata zote kamati ya Siasa imegawanyika makundi sita ambapo ziara hiyo itakuwa na vikao vya ndani vya chama na badae mikutano ya hadhara ya wananchi ikiwa na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili" alisema Mabihya.
Katibu huyo alisema kuwa, ziara hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi ambapo pia viongozi hao watakagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.
Aidha ziara hiyo itatumika kukumbushana na wananchi juu ya mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hasani katika sekta mbalimbali ikiwamo Afya, Elimu, Maji, Miundombinu pia itasaidia kuimarisha chama na kukumbushana wajibu wa wanachama na wananchi.
"Tutatumia ziara hii pia kuendelea kwa chama na viongozi na wanachama kuyaishi maadili ya Chama ambapo miongozo hiyo inapatikana kwenye Katiba ya Chama ili kuyaishi na kuyasimamia" alisema Mabihya.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara itakayokuwa imepangwa ili kusikiliza mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita pamoja na kupata majibu ya changamoto zinazowakabili.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...