Na Muhidin Amri,
Mbinga
SERIKALI imetoa Sh.milioni 331,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kata ya Matarawe Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye shule ya msingi Kipika.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kipika Kosmas Ndunguru alisema,katika mradi huo unaotekelezwa kupitia fedha za mpango maalum wa Boost wamefanikisha kujenga vyumba tisa vya madarasa ambapo madarasa saba kwa ajili ya elimu ya msingi na mawili ya elimu ya awali.
Kwa mujibu wa Ndunguru,fedha hizo zinahusisha ujenzi wa matundu 16 ya vyoo,lakini kutokana na usimamizi mzuri wameongeza matundu mengine mawili kwa ajili ya walimu na hivyo kuwa na jumla ya matundu 18.
Mwalimu Ndunguru alisema,kukamilika kwa ujenzi wa shule mpya kutasaidia kupunguza adha kwa wanafunzi kukaa zaidi 100 katika chumba kimoja na kuwawezesha walimu kuwafikia watoto wote kwa wakati mmoja na kuinua taaluma.
“shule ya msingi Kipika ina jumla ya wanafunzi 1,378 ambao ni wengi kuliko uwezo wa vyumba vya madarasa vilivyopo,kwa hiyo kujengwa kwa shule mpya kutafanya kila darasa kuwa na watoto arobaini tu”alisema Ndunguru.
Ametaja kazi zinazoendelea kufanyika kwa sasa ni ufungaji wa madirisha na kupaka rangi kwenye vyoo,ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia fedha ambazo zitatumika kuinua kiwango cha taaluma na kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.
Gradness Kayombo mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kipika alisema,madarasa mapya yatawawezesha kuwa na uelewa darasani na kukaa kwa nafasi, tofauti na awali ambapo walikaa kwa taabu jambo lililosababisha kushindwa kuandika vizuri na kukosa usikivu wa kile wanachofundishwa na walimu wao.
Kayombo alisema,watatumia madarasa hayo mapya kusoma kwa bidii ili waweze kufanikisha ndoto zao na kuhaidi kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Elisha Nyoni,ameishukuru serikali kuwajengea shule mpya ambayo ikikamilika itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuhamasisha wanafunzi wengi kupenda kuhudhuria shule.
Kassian Nombo mkazi wa kata ya Matarawe alisema,katika kata hiyo kuna shule moja tu ya msingi ambayo inakabiliwa na changamoto ya kuwa na idadi kubwa ya watoto,kwa hiyo shule mpya itasaidia wanafunzi kukaa kwa nafasi na kusikiza wanayofundishwa na walimu.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kipika Kosmas Ndunguru wa tatu kushoto akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ujenzi,wazazi na wataalam kutoka Halmashauri ya Mji Mbinga waliotembelea kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo mpya.Baadhi ya vyoo vya shule hiyo vikiwa katika hatua ya mwisho kukamilika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...