Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Singida, Peter Njau (kulia) akitoa elimu ya kupinga ukeketaji kwa wananchi katika mnada wa Kijiji cha Nkwae Kata ya Msisi uliofanyika Oktoba 3, 2023 kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP)


Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) lenye makao yake makuu Dodoma linalojishughulisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto na utoaji wa msaada wa kisheria bure kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida limetoa elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji kwa wananchi katika Mnada wa Kijiji cha Nkwae unaofanyika kila mwezi Kata ya Msisi.

Kupitia ufadhili wa Shirika la Women Action Against FGM (WAAF) Japan shirika WOWAP wanatekeleza mradi wa kupinga ukeketaji kwa kutoa elimu katika makundi ya jamii kwenye wilaya hiyo.

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Singida, Peter Njau akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utoaji elimu katika mnada huo alisema wilaya humo bado kunachanga changamoto kubwa ya ukeketaji na kuwa licha ya kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo dhidi ya watoto wa kike na wanawake uelewa wa jamii ni mdogo.

“Jamii ya maeneo haya bado inauelewa mdogo na inaendelea na vitendo vya ukeketaji ndio maana shirika la WOWAP limeanzisha kampeni ya kuzunguka kwenye kila mnada kwa ajili ya kutoa elimu hii ambayo tunaamini itawafikia watu wengi zaidi kwa wakati mmoja,” alisema Njau.

Alisema elimu hiyo imekuwa ikiwahusisha viongozi wa dini, wazee maarufu, wanafunzi, wanawake, viongozi wa vijiji na kata, wakunga wa jadi na ngariba wastaafu.

Njau alisema kampeni hiyo ni endelevu na itakuwa ikifanyika katika kila mnada wilayani humo lengo ni kuhakikisha vitendo hivyo vinakwisha kama sio kumalizika kabisa.

Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo, Felix Maigo alisema vitendo vya ukeketaji vinafanyika kutokana na sababu za kidesturi, dini, kuhifadhi utamaduni, bikra, usafi, kulinda heshima ya familia na kukubalika kwenye jamii haswa kuhusiana na ndoa.

Akielezea ukeketaji alisema ni ukataji wa sehemu za siri za mwanamke ambao unahusisha maeneo nyeti na kuwa aina ya kwanza ya ukeketaji ni kuondolewa kwa kinembe (kisimi) na kuwa aina ya pili ni kuondolewa kwa sehemu au jumla ya kisimi na midomo ya ndani ya uke.

Alitaja sehemu ya tatu kupunguza au kukata kwa ujumla uke na nne ni taratibu zote zenye madhara ikiwa ni pamoja kukata, kuchoma, kurarua, kutoboa na kutanua sehemu za siri za uke.

Alisema hivi sasa ukeketaji kwa watoto hufanyika kwa siri kubwa kwa wahusika kuogopa kufikiwa na mkono wa sheria kutokana na vyombo mbalimbali vya dola na mashirika yasiyo ya kiserikali kupigia kelele jambo hilo.

Maigo alitaja baadhi ya madhara ya ukeketaji kuwa ni makubwa ikiwa na kusababisha kifo kutokana na mfanyiwaji kutoka kwa damu nyingi na maumivu makali, uharibifu wa mfumo wa nje wa viungo vya uzazi, na maambukizi, msongo wa mawazo, kupungua hamu ya kufanya mapenzi, kuongeza hatari ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, watoto kuzaliwa kabla ya muda, kuongezeka kwa vifo vya uzazi na madhara mengine mengi yanayofanana na hayo.

Maigo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa kila mwana jamii katika eneo analoishi kupiga vita vitendo hivyo vya ukeketaji na kutoa taarifa kwa kupiga bure namba ya simu 116.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Maghojoa, Godwin Mgitu alisema moja ya kazi kubwa wanayoifanya ni utoaji wa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili katika kata hiyo na vinapotokea wahusika uchukuliwa hatua na alilipongeza shirika hilo kwa hatua walioichukua ya kuanzisha kampeni hiyo ya utoaji wa elimu kwenye minada.

“Niliwaombe WOWAP warudi tena kutoa elimu hii ili wananchi waweze kuelewa zaidi kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo katika maeneo yetu,” alisema Mgitu.

Mkazi wa Kijiji cha Kinyagigi, Amiri Jumanne alisema hivi sasa vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma alilishukuru Shirika la WOWAP kwa kuanziasha kampeni hiyo ya kutoa elimu kwenye minada na kueleza kuwa ni nzuri na itawafikia watu wengi hasa katika maeneo ya vijijini.

“Kipekee nilishukuru shirika la WOWAP kwa kazi hii kubwa wanayoifanya pia nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji,” alisema Jumanne.

Mkazi wa Maghojoa Mrisho Ramadhan alisema vitendo hivyo havikubaliki hata kidogo hivyo aliliomba shirika hilo kuifanya kampeni hiyo ya kutoa elimu minadani kuwa endelevu.

Mrisho alisema moja ya majukumu yao kama viongozi wa dini ni kukemea vitenndo hivyo katika maeneo yao ya ibada na kuwa wanapata mafanikio baada ya jamii kuonesha kubadilika.Wananchi wengine walioipongeza kampeni hiyo ni Saimon Ghalanda, Khalidi Samwel na Zaituni Salim kutoka Kijiji cha Msimii.


Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo, Felix Maigo, akitoa elimu katika mnada huo.

Wananchi wakipata elimu kupitia vipeperushi.

Wanawake waliokuwepo kwenye mnada huo wakipata elimu kupitia vipeperushi vinavyo kataza ukeketaji na kuonesha madhara yake.

Vipeperushi vikisomwa.

Elimu kwa njia ya vipeperushi ikifanyika.

Mzee Mrisho Ramadhan ambaye ni kiongozi wa dini akizungumzia jinsi wanavyoshughulikia vitendo vya ukatili katika maeneo yao ya ibada.
Mkazi wa Kijiji cha Kinyagigi, Amiri Jumanne akizungumzia kupungua kwa vitendo vya ukeketaji baada ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali NG'OS kutoa elimu.

Wananchi wakiwa katika Mnada wa Ghata ambapo walipatiwa elimu ya kupinga ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake.Ukeketaji na ukatili mwingine wa kijinsia ukipingwa.

Mkazi wa Kata ya Maghojoa, Khalid Samuel akilishukuru Shirika la WOWAP kwa kuwapelekea elimu hiyo.

Zaituni Salim kutoka Kijiji cha Msikii akipinga vitendo vya ukeketaji na ukatili mwingine ambao alisema bado upo katika maeneo hayo.

Rashid Ally akizungumzia ukeketaji na kueleza haukubaliki kabisa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...