Na Said Mwishehe, Michuzi TV

JUMUIYA ya Watu wanaoishi na Sikoseli imetoa huduma za upimaji ugonjwa wa Sikoseli bure kwa wananchi wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani sambamba na kuendelea kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Kambi hiyo ya upimaji Sikoseli,Presha na Sukari  imefanyika Viwanja vya Chanzige wilayani Kisarawe na upimaji huo ulifanywa na timu ya watalaam wa afya wakiongozwa na Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza katika wilaya hiyo Almas Katumba .

Akizungumza na Michuzi Blog Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Sikoseli Arafa Saidi amesema wamefika Kisarawe kwa lengo la kuadhimisha mwezi wa uelewa wa Sikoseli ambao ni mwezi wa tisa

“Kitaifa Septemba ni mwezi wa kuongeza uelewa kwa wagonjwa Sikoseli, tumekuja kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Sikoseli lakini kuhakikisha watu wanatambua hali zao na ugonjwa wa huu.

“Pia tuko hapa kutoa elimu na kupima baadhi ya magonjwa yasiyoyakuambukiza.Kama  mnavyojua magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi,”amesema.

Kuhusu mwitikio amesema wananchi wengi wamefika kupima sukari, presha na Sikoseli na wengi wao wameuliza maswali kwa lengo la kufahamu zaidi kuhusu ugonjwa huo.

“Tuna deni kubwa bado kwasababu elimu haijafika kwa watu wengi zaidi , hivyo jumuiya yetu na wadau wote tunayo sababu ya kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu kuhusu Sikoseli,”amesema.

Amefafanua kauli mbiu yao ni kuvunja mduara wa Sikoseli ili watu wajitambue mapema kabla ya kuanzisha familia au kama wameanzisha basi watakuwa wanajielewa hali zao mapema.

Kuhusu changamoto watu kuanzisha familia bila kupima Sikoseli , amesema kama hawajajitambua halafu wakapata mtoto ambaye tayari amepata huo ugonjwa shida inakuja kwanza watu kufahamu ugonjwa umetokea wapi au umeanzia wapi.

“Kunakuwa na sintofahamu kwasababu wengi hawajui kama Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi ,kwa hiyo wengi wanauweka katika kurogwa na wakati mwingine inasababisha ndoa kuvunjika.”

Alipoulizwa kuhusu uelewa  wa  watu, amejibu mara nyingi watu wanaposikia Sikoseli wanahisi ni ugonjwa wa mifupa au damu, kwa hiyo wengi ambao wanauzungumzia wanahisi kuwa wametupiwa majini kwasababu damu inaisha mara kwa mara.“Wanakuwa na uelewa huo kwasababu wengi hawajui kama Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi.”

Akizungumzia ndoa kuvunjika kwasababu ya mtoto kuwa na Sikoseli, amesema kumekuwepo na kesi nyingi wanaume wanawaacha wamama na moja ya sababu mwanaume anaamini huenda mama alichepuka na hivyo kumpata mtoto mwenye ugonjwa huo.

“Watoto wengi wamerithi Sikoseli lakini  kwasababu wengi wanakuwa hawaelewi na wanahisi labda mama alichepuka sababu mara nyingi wanasema jamii inafikiria lazima kuwe na kiashiria ama kwa baba au mama.

“Kwa hiyo wapo wanawake wengi ambao tunakutana nao wako peke yao kwasababu wababa wamekimbia kwa kutokufahamu kwamba changamoto lazima itoke kwa baba na mama na ndio maana tunasema tuzidishe elimu ili kuisaidia jamii kuutambua ugonjwa huu na nini chanzo chake.”

Kwa upande wake mmoja ya wananchi wa Kisarawe Joyce Nyoka anayeishi mtaa wa Bomani amesema amefika katika kambi hiyo ya vipimo kutokana na kuona mwanaye anasumbuliwa na malaria na damu kupungua mara kwa mara.

“Baada ya kusikia tangazo kutakuwa na upimaji wa Sikoseli nikaona nije leo nimlete mtoto wangu apime  ili nijue kama anao ugonjwa au hana. Bahati nzuri amegundulika hana Sikoseli.“Wamenipa ushauri .”

Ameongeza baada ya majibu hayo anakwenda kuwatangazia mtaani kwake kwani kulikuwa na maneno mengi ya watu wakimsema mtoto wake kuwa ana Sikoseli, hivyo ni wakati wake kwenda kuwaambia kuwa mtoto wake hana ugonjwa huo.

“Majirani walikuwa wanamtangaza mwanangu ana Sikoseli.”amesema na kutoa rai kwa jamii kuacha kunyanyapaa watoto wenye Sikoseli.

 

JE SIKOSELI NI NINI?

Ni ugonjwa wa kurithi wa kupungukiwa damu ambapo mgonjwa huwa hana damu ya kutosha kwasababu ya seli zake za mwili sio imara kubeba hewa ya oksijen kupeleka sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa hali ya kawaida seli za binadamu huwa na umbo la kama yai na linalovutika kiasi kwamba huweza kupita kirahisi katika mishipa ya damu na seli hizo kuishi siku 120 yaani miezi mitatu kisha hufa kupisha zingine.

Lakini seli za mgonjwa Sikoseli ni ngumu yaani zipo kama shepu ya mwezi na huishi siku 20 tu na huweza kukwama kwenye mishipa ya damu na kuzuia damu kupita na hicho ndicho chanzo kikuu cha matatizo

Wagonjwa wa Sikoseli husumbuliwa na mashambulio ya maumivu mara kwa mara sababu ya kukwama kwa seli hizo na kuzuia oksijeni kwenda sehemu za viungo vya mwili.

CHANZO CHA UGONJWA HUO NI NINI?

 Ugonjwa huo husababishwa na kubadilika kwa mfumo wa mwili wa kutengeneza vimelea vya kutengeneza damu yaani haemoglobin .Haemolgobin hiyo  husababisha seli zinazotengenezwa kuwa na shepu ambayo sio ya kawaida.Ugonjwa huo hurithiwa kutoka kwa wazazi wote yaani baba na mama ,kitalaam wanaita

carriers.

Hivyo Mama na baba wanaweza kuwa hawana dalili yeyote lakini wamebeba vimelea vya ugonjwa huo katika damu zao na kumzaa mtoto mgonjwa.

Mgonjwa sikoseli akioa au akiolewa na mtu ambaye sio mgonjwa hawezi kuzaa wagonjwa ila atazaa watoto wenye vimelea hivyo wakiona wanaweza kuzaa mtoto mgonjwa .

Inaelezwa mume na mke wagonjwa wakioana watazaa wagonjwa watupu hivyo ni vizuri kuangalia mapema kabla ya kuamua kuzaa.

DALILI ZA UGONJWA HUO NI ZIPI?

 
Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalam ni kwamba mgonjwa wa Sikoseli haoneshi dalili yeyote mpaka afikishe miezi minne ya umri tangu kuzaliwa na huanza na dalili zifuatazo kama kuishiwa damu,Maumivu makali ya mwili Kuvimba vidole , kuchelewa kukua kwa watoto, kutoona vizuri .

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Sikoseli  Arafa Said(wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wakati wa kambi ya upimaji Sikoseli iliyofanyika viwanja vya Chanzige wilayani Kisarawe mkoani Pwani
Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza Wilaya ya Kisarawe Almas Katumba akiendelea na kutoa huduma ya vipimo kwa mmoja ya wananchi wa Wilaya hiyo

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Sikoseli  Arafa Said ( kushoto) akijadiliana jambo na Mratibu wa Magonywa yasiyoyakuambukiza Wilaya ya Kisarawe Almas Katumba




Matukio mbalimbali katika picha wakati wa upimaji ugonjwa wa Sikoseli kwa wananchi wa Wilaya ya kisarawe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...