WANAFUNZI 110 wenye mahitaji maalumu katika sekondari ya Jangwani wamepewa msaada wa vifaa vya usafi, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Jangwani, jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2023, Mtaalamu wa Miradi wa Shirika la WaterAid, Rebecca Stanley, amesema wamekabidhi vifaa mbalimbali ili kuimarisha afya kwa wanafunzi wenye changamoto shuleni hapo.

“Leo tunakabidhi mahitaji haya yenye thamani ya Sh. milioni sita kwa wanafunzi hawa wenye uhitaji maalumu kwa ajili ya kuwasaidia kwenye masuala ya usafi binafsi na wa mikono,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Wanawake, wasichana na watu walio katika makundi maalumu ni makundi ambayo tunayapa kipaumbele kikubwa sana katika kazi tunazozifanya.”

Akipokea vifaa hivyo, Ofisa Afya wa Manispaa ya Ilala, Reginald Mlay, ameishukuru WaterAid Tanzania kwa kujumuika na wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika maadhimisho hayo.
Ameishukuru pia kwa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusiana na umuhimu wa unawaji mikono na usafi binafsi kwa ujumla.

“Tunashukuru sana Shirika la WaterAid, mbele yetu leo tumepokea sabuni za kunawia mikono, sabuni za kusafishia choo, vifaa vya kuhifadhia sabuni, sabuni za kuogea, sabuni za kufulia pamoja na taulo za kike na ndoo za kunawia mikono, tunaamini mahitaji haya yatawasaidia sana wanafunzi hawa katika masuala mazima ya usafi,” amesema Mlay.

Siku ya kunawa mikono duniani huadhimishwa Oktoba 15 kila mwaka na mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu ya ‘mikono safi inaweza kufikiwa.’

Shirika la WaterAid Tanzania linashiriki maadhimisho ya siku ya kunawa mikono miezi michache baada ya kuadhimisha miaka 40 ya utendaji kazi hapa nchini.

Dhima ya Shirika hilo la kimataifa ni kuhimiza upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo bora na huduma za usafi, ili kuwaepusha wananchi na magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji na uchafu.
WaterAid inafanya kazi katika nchi 28, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika.




Sehemu ya vifaa vya usafi vilivyokabidhiwa



Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakipewa elimu ya usafi na ofisa wa Shirika la WaterAid (hayupo pichani), wakati wa maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani.


Mtaalamu wa Miradi wa Shirika la WaterAid, Rebecca Stanley, akikabidhi taulo za kike kwa mmoja wa wanafunzi wa sekondari ya Jangwani

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...