Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso amezitaka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana kumsimamia mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya Kilwa Masoko Mkoani Lindi ili ukamilike kwa wakati na viwango.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo mkoani Lindi Mwenyekiti Kakoso amesema bila kuwa na mkakati madhubuti wa usimamizi kwenye ngazi zote za utekelezaji thamani ya fedha haitoonekana baada ya mradi kukamilika hivyo kazitaka Wizara hizo kuongeza nguvu kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara.

“Serikali inatoa fedha nyingi katika kutekeleza miradi lakini changamoto iliyopo wakandarasi wanaotekeleza miradi hii hawasimamiwi kwa karibu sasa nyinyi mna wataalam wa kutosha waleteni hapa wakague kazi zinazoendelea kila siku maana tunataka kuona thamani ya fedha zilizowekezwa kwenye mradi huu’ amesema Mwenyekiti Kakoso.

Mwenyekiti Kakoso amesema pamoja na ujenzi huo Wizara hizo zihakikishe miradi ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) iliyopangwa kutekelezwa inazingatia mahitaji ya wahusika ili wananchi wapate manufaa zaidi kwenye maeneo nje ya uwekezaji huo wa bandari.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wavuvi kufanya biashara kwa urahisi kwani umezingatia mahitaji yote ikiwemo miundombinu ya kutunzia na kuhifandhi bidhaa za Samaki kabla ya kusafirishwa kwa watumiaji wa ndani na nje ya Nchi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara amemuhakikishia Mwenyekiti Kakoso tayari TPA imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba.

Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilion 250 na unatarajiwa kukamilika Februari, 2025 ambapo kukamilika kwake kutaifanya Tanzania kuwa na Bandari ya kwanza ya uvuvi ambayo itakuwa kichocheo cha uchumi, kuongeza ajira na upatikanaji wa Samaki wa lishe na kuongeza mapato ya Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Seleman Kakoso akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Mkoani Lindi, mwishoni mwa wiki.

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile akisisitiza jambo kwa Mwenyekiti na Wajumbe Kamati ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa kwenye usimamizi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, wakati kamati hiyo ilipotembelea bandari hiyo mkoani Lindi mwishoni mwa wiki.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara akitoa maelezo kwa Mwenyekiti na Wajumbe Kamati ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu maeneo yaliyozingatiwa katika ujenzi wa  ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, wakati kamati hiyo ilipotembelea bandari hiyo mkoani Lindi mwishoni mwa wiki.

PICHA NA WIZARA YA UCHUKUZI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...