Wandaaji wa toleo la 22 la Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 leo wameitangaza Gee Soseji kama mdhamini mpya wa mbio za kujifurahisha za kilomita 5, mbele ya tukio lenyewe litakalofanyika Februari 25, 2024.

Taarifa iliyotolewa na waandaji Dar es Salaam inasema wamefurahi sana na wanawakaribisha Gee Soseji kwa nafasi hiyo, ikiongeza kwamba mbio hizi za Km 5 sasa zitajulikana kama Gee Soseji 5km Fun Run.

“Mbio za Kilomita 5 ni shindano kubwa linalowavutia zaidi ya wakimbiaji 5,000, hivyo Gee Soseji watapata umaarufu na kujulikana zaidi kutokana na udhamini huu mpya na ni matumaini yetu kuwa huu utakuwa uhusiano wa muda mrefu ambao utapeleka shindano hili kwa ngazi nyingine,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Kilimanjaro Marathon.

Wandaaji pia waliyasihi makampuni mengine na mashirika kuona na kutumia fursa nyingine za ufadhili zinazohusiana na tukio hili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Gee Soseji Bw.David Minja alisema wanaona fahari kushirikiana na Kilimanjaro Marathon, moja ya matukio makubwa ya michezo katika ukanda huu.

“Kwetu sisi, hili ni jukwaa sahihi la kutangaza bidhaa zetu, kuwa pamoja na wateja katika burudani na kuwaelimisha watu juu ya lishe bora na jinsi ya kuwa na mtindo mzuri wa maisha,” alisema Bw Minja.

Alisema timu za matangazo za Gee Soseji zitakuwa Moshi kwa takriban juma moja kabla ya mbio za masafa marefutukio la Kilimanjaro Marathon na kukutana na wateja katika sehemu mbalimbali kama vile kwenye baa na sehemu nyinginezo na kuhakikisha wanapata uzoefu wa kuonja Gee Soseji na kushirikishana faida za lishe bora.

“Tunakusudia pia kutumia udhaminii huu kuzindua Gee Soseji na kuhakikisha zinapatikana Moshi, Arusha, Mbeya, Mwanza na hatimaye Tanzania nzima na duniani kote,” alisema.

Aliwasihi washiriki wa mbio za kilomita 5 kujiandikisha kwa wingi kwa vile kwa sasa wana kitu zaidi cha kutarajia kabla, wakati na baada ya mashindano yenyewe. “Tutapeleka basi kupakia wafanyakazi, wateja na wacheshi kushiriki na kuburudika,” aliongeza.

Wafadhili wengine ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager (mfadhili mkuu) na Tigo –Mfadhili wa Mbio za km 21- Kili Tigo 21km Half Marathon, wadhamini wa meza za maji, Simba Cement, Kilimanjaro Water na TPC Sugar. Wabia rasmi ni KiliMedair, Garda World Security, CMC Automobiles, Sal Salinero Hotel na wasambazaji rasmi – Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na Executive Solutions Ltd.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...