Na Mwandishi Wetu
Miss Tanzania 2022 Halima Ahmad Kopwe kwa kushirikiana na Coral Paints ametoa msaada wa rangi kwa ajili ya ukarabati wa jengo la watoto katika hospitali ya Tumbi wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine Duniani katika kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani Ijumaa Novemba 17, 2023.
Akiongea wakati wa kukabidhi msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili, Mlimbwende huyo alitoa wito kwa jamii kuwatunza vema watoto wanaozaliwa kabla ya muda ili kuokoa maisha yao, wakue vizuri na kuwa na tija katika jamii.
”Natoa wito kwa jamii kusikiliza ushauri wa watalaamu wa afya katika kuhakikisha watoto hawa wanatunzwa vizuri, ikiwemo kutoa elimu kwa akina mama kuwapa joto la kutosha watoto wanaowazaa kupitia uleaji wa Kangaroo kwa kuwakumbatia ili kuwapa joto linalotakiwa,”amesema.
Akiwa kama kioo katika jamii, amesema kuwa amekuwa akishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo kampuni ya Insignia Limited, wazalishaji wa rangi za Coral Paints na Galaxy katika kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji.
”Urembo wangu unatakiwa uwe na manufaa kwa jamii inayonizunguka na ndio maana nashirikiana na wadau ili kuwapa faraja na tabasamu wale wanaohitaji,”
" Nawashukuru sana Coral Paints, waliitikia wito wa kutoa msaada nilipowaomba kwa ajili ya ukarabati wa jengo la watoto," amesema mrembo huyo.
Naye Meneja wa Masoko wa kampuni hiyo Adam Kefa amesema kampuni yake kupitia bidhaa zake za rangi bora imekuwa ikisaidia jamii katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya.
”Ni faraja kwetu kushirikiana na Miss Tanzania na kutoa msaada huu kwa watoto njiti, ambao ni sehemu ya tarajio la nchi katika kukuza uchumi hapo baadae,”
”Rangi hizi tulizozitoa, mbali ya kukarabati majengo ya wodi za watoto, pia zitasaidia kukuza akili zao kwa sababu rangi siku zote zinavutia kwa watoto na kuwapa furaha muda wote,” amesema Kefa.
Mbali na ugawaji wa rangi hizo takriban ndoo 19 za lita 20 na mifuko ya kuskimia ukuta, Miss Tanzania pia alishiriki katika maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika Novemba 17, 2023 kwa kupewa maelezo na wataalamu juu ya namna ya uleaji bora wa watoto hao na baadae alitoa zawadi mbalimbali kwa wahudumu wa wodi ya watoto wakiwemo wakunga na wazazi.
Mmoja wa wazazi hao, Tatu Issa amesema yeye alizaa mtoto njiti mwenye gramu 900, lakini baada ya kufuata ushauri wa watalaamu, mtoto wake amekuwa vizuri sana kimwili na kiakili na sasa hivi ana umri wa miaka 6.
”Nawashukuru sana wahudumu wa Hospitali ya Tumbi wanaotufanya wazazi wa watoto njiti tuwe na matumaini ya ukuaji wa watoto wetu,” amesema.
Naye Daktari wa wodi hiyo Janeth Olwal, ambaye naye alizaliwa njiti amesema jamii inapaswa kubadili mtazamo juu ya watoto hao kwa sababu hawana tofauti na watoto wengine, ila tofauti tu wao wanazaliwa kabla ya wakati (Premature).
”Mimi mwenyewe nilizaliwa njiti, lakini nimekuwa vizuri na hivi sasa ni daktari,” amesema.
Naye Maryam Ali Khamis, Afisa Muuguzi Msaidizi amesema wanatoa elimu kwa wazazi wa watoto njiti juu ya namna ya kuwalea , ikiwemo unyonyeshaji na ukumbatiaji.
Kitaifa, katika kuadhimisha maadhimisho hayo, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua Mpango Harakishi wa Watoto Njiti na Watoto Wachanga.
Akizungumza katika Uzinduzi huo Jijini Dar Es Salaam katika Mkutano wa Pili wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, Mhe.Kikwete amesema tatizo la kuzaliwa watoto njiti hapa nchini ni kubwa ambapo kuna takriban watoto wachanga 300,000.
“Tatizo hili ni kubwa, kuna takriban watoto wachanga mia mbili hamsini elfu huzaliwa Tanzania kabla ya wakati, hivyo ni muhimu kuweka jitihada katika kupunguza hili”amesema Mhe. Kikwete.
Aidha, Mhe. Kikwete amesema maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila Hospitali inakuwa na Wodi maalum za Watoto njiti(NICU) hali itakayosaidia kuokoa maisha ya watoto .
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema lengo la Serikali ni kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya watoto wachanga ambapo ukiwa na kituo cha watoto wachanga inasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 50.
Miss Tanzania 2022 Halima Kopwe ( mwenye nguo nyekundu) akipokea sehemu ya msaada wa rangi za Coral Paints kutoka Kwa Meneja wa Masoko Adam Kefa ( kati kati) kwa ajili ya kukabidhi Kwa hospital ya Tumbi, Kibaha kitengo Cha watoto katika maadhimisho ya mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika Novemba 17, 2023.
Miss Tanzania 2022 Halima Kopwe ( mwenye nguo nyekundu) akipokea sehemu ya msaada wa rangi za Coral Paints kutoka Kwa Meneja wa Masoko Adam Kefa ( kati kati) kwa ajili ya kukabidhi Kwa hospital ya Tumbi, Kibaha kitengo Cha watoto katika maadhimisho ya mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika Novemba 17, 2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...