Nov 23

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKOA wa Pwani umekabidhi vishkwambi 345 kwa Maofisa Kilimo wa Wilaya ili kuleta tija na kuongeza mnyororo wa thamani.


Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa huo ,Abubakar Kunenge wakati akikabidhi vifaa hivyo ambavyo vimetolewa na Serikali.


Kunenge amesema, vitasaidia kusajili wakulima ambao bado hawajaingizwa kwenye mfumo na kuboresha taarifa za wale waliosajiliwa ili wahudumiwe kwa idadi na kujua mahitaji yao ya pembejeo.


"Ili kilimo kiwe na tija lazima wataalamu wawe na vifaa vya kisasa na hata iwe rahisi kutoa taarifa juu ya maendeleo ya kilimo au kama kuna changamoto," amesema Kunenge.


Amesema kuwa, kupitia vifaa hivyo wataweza kutoa taarifa sahihi za pembejeo kwa wakulima kuanzia afya ya udongo, mbegu bora, mabadiliko ya hali ya hewa na matumizi sahihi ya mbolea.


"Tunaipongeza Serikali kwa kutoa pikipiki 129, vifaa vya kupimia udongo sita na sasa Vishkwambi, hii inaonyesha jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kutaka kubadili kilimo kiwe na tija kwa wakulima na nchi," amesema Kunenge.


Aidha amesema , mkoa umepata mafanikio makubwa kwa sasa ambapo ubora wa zao la korosho ya daraja la kwanza umeongezeka kutoka asilimia 12 hadi 96.6.


"Zao la ufuta ubora na uzalishaji umeongezeka na tunaongeza nguvu kwenye mazao yakiwemo katani, mahindi, miwa, mihogo, chikichi, mpunga ,mbaazi pamoja na ndizi ambapo tayari kuna wawekezaji wakubwa wameshajitokeza,"


Amewataka maofisa hao kuongeza mnyororo wa thamani kupitia mazao ya kibiashara ambayo yanaongeza pato kwa wakulima.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kutoa taarifa mbalimbali kwa Wizara na kutoa elimu kwa wakulima juu ya masuala ya kilimo.


Naye Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Joseph Njau amesema kuwa vishkwambi hivyo vitawawezesha kutekeleza majukumu yao na kuongeza uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima kwenye maeneo yao.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...