Na Muhidin Amri,
Mtwara

ZAIDI ya wakazi 4,960 wa vijiji vitatu vya Njengwa,Majengo na Njengwa sokoni kata ya Njengwa wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara,wameondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kukamilisha mradi wa maji ya Njengwa-Majengo.


Akitoa taarifa ya mradi huo kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Abdulaaziz Hemed alisema,mradi huo umetekelezwa na wataalam wa ndani chini ya usimamizi wa Ruwasa wilaya ya Mtwara na muda wa utekelezaji ulikuwa miezi sita ambapo ulianza mwezi Februari na kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2023 kwa gharama ya Sh.milioni. 883.

Alisema,mradi huo ulihusisha ujenzi wa tenki la lita 100,000 katika mnara wa mita 9,ukarabati wa matenki madogo 2 yenye ujazo wa lita 50,000 kila moja,kujenga vituo vya kuchotea maji 8 katika kijiji cha Majengo na vituo 6 katika kijiji cha Njengwa na Njengwa sokoni.


“ kwa ujumla wakazi wa vijiji hivi tayari wameanza kutumia maji ya bomba baada ya Ruwasa kukamilisha kazi ya ujenzi wa mradi huu,sisi kama wakala wa maji tunamshukuru sana Rais wetu Mpendwa mama Samia Suluhu Hassan kutupatia zaidi ya Sh.milioni 800 zilizofanikisha kutekeleza mradi huu ”alisema Hemed.


Alisema,serikali imedhamiria kumaliza kabisa kero ya upatikanaji wa maji na kuwataka wananchi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanatunza miundombinu ya mradi pamoja na vyanzo vya maji ili mradi huo uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.


Aidha,amewataka wananchi kuanza kuingiza maji ya bomba kwenye nyumba zao ili kuepuka usumbufu wa kukaa kwenye vituo vya kuchotea maji kwa muda mrefu na hivyo kushindwa kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Mkazi wa kijiji cha Njengwa sokoni Said Hamis alisema,mradi huo umeleta nafuu kubwa katika maisha yao kwani hapo awali walitumia muda mrefu kwenda kutafuta maji kwenye mito licha ya kijiji hicho kuwa na vyanzo vingi vya maji.



“tulikuwa tunakwenda kutafuta maji kwenye mito na visima tulivyochimba kwa mikono mbali na makazi yetu, baadhi ya wenzetu walipatwa na matatizo makubwa kwa kushambuliwa na wanyama wakali wakiwemo fisi,chui na wengine kugongwa na nyoka,tunaishukuru sana serikali yetu kutujengea mradi huu”alisema Hamis.


Alisema,katika umri wake wa miaka 71 hajawahi kuona maji ya bomba katika kijiji hicho,lakini sasa amefurahi baada ya kushuhudia maji yanapatikana katika kijiji hicho na kumaliza mateso yaliyokuwepo kwa muda mrefu.



Kwa upande wake Diwani wa kata ya Njengwa Halmashauri ya wilaya Mtwara vijijini Moza Kapela alisema,tangu Uhuru mwaka 1961 wananchi wa kata hiyo hawajahi kuona maji ya bomba wala kuonya radha ya maji ya bomba.


Badala yake walikuwa wanatumia maji ya visima na mito au maji ya mvua na walikuwa wanatoka nyumbani kati ya saa 9 na 10 usiku na kurudi saa 12 alfajiri kutoka kutafuta maji hali iliyozusha migogoro mingi na ya mara kwa mara kwa baadhi ya familia.


Alisema,tangu serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani wananchi wa kata hiyo wamekuwa wenye amani na furaha kubwa hasa baada ya kushuhudia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji Njengwa.


Alisema,baada ya kukamilika kwa mradi huo sasa migogoro hasa inayohusu ndoa imepungua kwani wanawake wanatumia muda mfupi kwenda kuchota maji kwenye vituo vilivyojengwa karibu na makazi yao.


Ameshauri kuwa,ili mradi huo uwe endelevu ni lazima watumiaji wawe wengi na kuwataka wasimamizi jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) kushirikiana na Ruwasa kuhakikisha wanawaunganishia maji watu wengi badala ya kubaki na wachache.
MWISHO.

Diwani wa kata ya Njengwa Halmashauri ya wilaya Mtwara mkoani Mtwara Moza Kapela kulia na kamimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Mhandisi Abdulaazi Hemed katikati,wakimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Njengwa Subira Aziz.

T

enki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji lililojengwa  ili kuhudumia wakazi wa kijiji cha Njengwa na Majengo kata ya Njengwa wilayani Mtwara.
 

Baadhi ya watumishi wa Ruwasa wilaya ya Mtwara wakiongozwa na kaimu meneja wa Ruwasa mhandisi Abdulaaziz Hemed  kushoto,wakimsikiliza Diwani wa kata ya Njengwa Moza Kapela aliyetembelea mradi wa maji Njengwa-Majengo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...