Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Mabaraza ya Michezo kuendelea kuratibu na kufuatilia utendaji wa vyama vya michezo na kuhakikisha vinaendeshwa na kujiendesha kwa manufaa ya taifa.

Rais Samia amesema serikali inapoweka mazingira mazuri katika sekta ya michezo hutoa hamasa kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo kwa kuwekeza katika timu za vijana.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa hafla ya chakula cha mchana aliyoiandaa kuwapongeza wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu.

Timu ya Karume Boys imetwaa Kombe la Mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika nchini Uganda ambapo tangu miaka ya 1990 Zanzibar haijawahi kushinda katika mashindano hayo.

Vile vile Rais Samia amesema michezo hutoa fursa ya ajira kwa makundi mbalimbali hususan vijana hivyo viongozi hawana budi kuweka mipango endelevu na kuwekeza katika sekta hiyo.

Aidha, Rais Samia ameyataka Mashirikisho ya Soka Tanzania bara na Zanzibar kutumia mapato yanayotokana na viingilio vya mechi kufanya ukarabati wa viwanja badala ya kusubiri matengenezo makubwa ambayo yanaongeza gharama maradufu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kutoa msukumo mkubwa katika kukuza sekta ya michezo nchini ikiwemo kurudisha ligi ya Muungano.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wachezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 25 Novemba, 2023.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita wa Zanzibar katika picha ya pamoja na Wachezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 25 Novemba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Wachezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 25 Novemba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa ameshika Kombe la Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati chini ya Umri wa miaka 15 (CECAFA U-15) pamoja na Gloves ya Kipa bora wa Mashindano hayo yaliyofanyika nchini Uganda. Mhe. Rais Samia aliwaandalia hafla ya kuwapongeza Wachezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 25 Novemba, 2023.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Benchi la Ufundi la timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 25 Novemba, 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...