Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imezindua kampeni ya Lishe kwa vijana balehe yenye lengo la kuhakikisha kundi la vijana linaondokana na utapiamlo na hatimaye kutimiza malengo yao ya kuwa wanavyotaka.
Kampeni hiyo ya lishe kwa vijana balehe imezinduliwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lishe kitaifa yaliyofanyika wilayani Mkuranga mkoani Pwani na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe nchini.
Akizungumza kwa niaba Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyekuwa mgeni rasmi , Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowelle amefafanua maadhimisho ya siku ya lishe mwaka huu yamefanyika sambamba na kuzindua kamepni ya lishe kwa vijana balehe.
Amesema uzinduzi huo ni ishara ya Serikali kuitikia mwito wa kutekeleza kampeni hiyo ya wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika lengo likiwa kuhamasisha wadau wa lishe nchini kuweka kipaumbele katika masuala ya lishe kwa kutenga bajeti ya lishe ya vijana balehe.
“Ili kutekeleza kampeni hii ninawaelekeza viongozi wote katika sekta zote kushirikiana na wadau pamoja na jamii kwa ujumla ili sasa kuhakikisha wanaboresha lishe ya vijana balehe…
“Kwa kutenga bajeti na kutekeleza afua za lishe zinazolenga kuimarisha hali ya lishe kwa vijana balehe shuleni na wale walio nje ya shule.”
Kuhusu maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa Meja Gowelle amesema yamekuwa yakifanyika kila Oktoba 29 kila mwaka na lengo la kuanzishwa siku ya lishe ni kuleta pamoja wadau wa lishe ili kuongeza uelewa kuhusu lishe kama msingi wa afya bora na maendeleo ya kiuchumi.
“Maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yamelenga kuchangia kuelewa na kufahamu kuhusu lishe bora na hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi wote ili kuleta mabadiliko chanya ya tabia za kilishe hususani katika ngazi ya kaya na jamii ili kupunguza utapiamlo nchini.
“Kila mwaka maadhimisho ya lishe kitaifa huja na kauli mbiu mahususi na kwa mwaka huu 2023 kauli mbiu inasema lishe bora kwa vijana balehe chachu ya mafanikio yao ,”amesema.
Amefafanua kauli mbiu hiyo inalenga kutokomeza utapiamlo nchini na taifa lenye watu wenye afya bora na wenye uwezo wa kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia , jamii na taifa kwa ujumla
Amesisitiza lishe bora ni msingi wa uhai , ukuaji na maendeleo ya binadamu kimwili na kiakili, kwani husaidia kuongeza uwezo wa ufanyaji kazi na hivyo kuongeza tija
“Wote mnajua ili tuweze kuleta maendeleo na kufikia uchumi wa viwanda katika nchi ni lazima tuwe na taifa lenye watu wenye lishe na afya bora.
“ Kwa upande mwingine utapiamlo huchangia kwa kiasi kikubwa kiwango cha umasikini kwa kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya mara kwa mara , kudhoofisha makuzi ya watoto na vijana balehe kiakili na kimwili.”
Meja Gowelle amesema pia utapamlo huongeza gharama za matibabu na kupunguza nguvu kazi ya ushiriki katika uzalishaji mali na hivyo kuathiri kipato na uchumi cha mtu mmoja mmoja , familia na jamii kwa ujumla.
Aidha amesema ni ukweli usiofichika hakuna taifa linaloweza kuendelea bila kutegemea vijana wake pamoja na ukweli huu kundi hilo linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya utapia mlo inayotokana na lishe pungufu na upungufu wa madini pamoja na vitamin
Amesema nchini Tanzania Serikali kwa kushirikiana na wadau wa lishe imeendelea kufanya jitihada kuboresha hali ya lishe ikiwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia sera ,miongozo na mikakati ya afua ikiwemo huduma za lishe.
Pia juhudi mbalimbali zimeendelea katika kuimarisha afya na ustawi wa vijana balehe kwa kuweka vipaumbele kwenye maeneo yanayolenga kutoa matokeo chanya nay a haraka.
“Miongoni mwa juhudi ni pamoja na kuandaa mpango jumuishi wa kitaifa wa lishe namba mbili wa 2021/2022 -2025-2026 na ajenda ya kitaifa ya kuharakisha hatua na uongezaji wa afya ya ustawi ya vijana 2021/2022 na 2024/2025 ambapo lishe ya vijana balehe imepewa kipaumbele.
Aidha Serikali kwa kushirikiana na wadau inatekeleza muongozo wa kitaifa wa utoaji huduma ya chakula na lishe shuleni inayolenga kuhakikisha alau mwanafunzi anapata japo mlo mmoja.
Hiyo ni kama kiasharia kwenye mkataba wa lishe ambao Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewasainisha wakuu wa mikoa yote nchini huku akifafanua utekelezaji unaendelea.

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...