Na Karama Kenyunko Michuzi Tv.

SERIKALI imewasisitiza wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu ikiwemo Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU), kuhakikisha wanazidi kuimarisha ubora wa elimu ya vyuo vikuu na kutokubali ushuke kwa namna yoyote ile.

Pia imesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu barani Afrika kuendeleza ushirikiano zaidi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema hayo leo Novemba 28, 2023 jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la kitaifa la mtandao wa wathibiti ubora wa elimu ya juu barani afrika (AfriQAN) linalofanyika katika hoteli ya Serena.

Kongamano hilo la 14 ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania lenye lengo la kujadili mchango wa uthibiti ubora katika kuongeza umahiri wa elimu ya juu Barani Afrika linahudhuriwa na washiriki mbali mbali kutoka nchi 22 barani Afrika, wakijimuisha, Taasisi za Uthibiti Ubora wa elimu ya juu, Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu Jumuiya na Asasi za Kimataifa na Kikanda zinazojihusisha na Elimu ya Juu Wanataaluma, Mabaraza na Bodi za Usajili wa Wataalam, na Wadau wa Elimu ya Juu kutoka ndani na nje ya nchi

Amesema, kumekuwepo na shinikizo la kushusha ubora siku zote lakini lazima wahakikishe ubora utakaofikiwa hatutofautiani na nchi nyingine yoyote duniani.

"Tuendelee kuimarisha ubora katika vyuo vikuu na tusikubali kushusha ubora kwa namna yoyote ile," amesema Mkenda na kuongeza kuwa uendeshaji wa vyuo vikuu ni biashara yenye ushindani hivyo basi vinapaswa kuhakikisha kuwa vinawasaidia wanafunzi Ili waweze kufanya vizuri na kukubalika katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi ".

Aidha amesema vyuo vikuu pia vinapaswa kuzingatia vigezo wakati wanapotaka kuajiri wahadhiri na wasishushe viwango vya kuajiri kwa lengo la kuonesha kuwa chuo kina maprofesa wengi.

Alieleza maeneo muhimu ya washiriki hao kuyajadili ni pamoja na uendeshaji wa vyuo vikuu kwani ni biashara yenye ushindani mkubwa.

"Kuna swala kila mtu analizungumzia kuwa tumeongeza idadi ya wanafunzi wengi wa vyuo vikuu lakini swala la ajira limekuwa changamoto, kwahiyo vyuo vikuu vinapaswa kupimwa ubora wake pia kupimwa ni kiasi gani vinamuandaa mwanafunzi aweze kujiajiri au kuajirika kirahisi amesema Prof. Mkenda.

Amesema viwango lazima viwe vya kimataifa kwani jambo hilo siyo kwa nchini tu, bali kwa Afrika nzima.

“Pamoja na hilo, lazima tuangalie kwamba hatushushi uwezo wa wanafunzi kufikiri kwa kuwa ukifanya hivyo watakuwa wameenda kusoma tu mambo ya ufundi, chuo kikuu kinapaswa kumfanya wanafunzi awe na uwezo wa kufikiri.

“Kuna umuhimu wa kushirikiana kuongeza ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania, lakini vya Afrika ni muhimu zaidi kushirikiana kwa sababu tunapishana katika maeneo kadhaa,” amesisisitiza.

Waziri Mkenda alisema chuo kikuu kazi yake siyo tu kurithisha uelewa, bali kuzalisha uelewa mpya na kufanya utafiti kwani utafiti kwa chuo kikuu ni jambo muhimu kwa kuwa hauwezi kuwa profesa kwa kutoa mhadhara tu, lazima uwe unaenda kufanya utafiti.


Pia vyuo vishirikiane kufanya tafiti kutatua matatizo ya wananchi kwa kuwa chuo kikuu ni taasisi ya utafiti na kufundishia huvyo wahakikishe wanapoongeza idadi ya wanafunzi, hawapunguzi muda wa wahadhiri kufanya utafiti.

Aidha amesisitiza nchi za Afrika kushirikiana na kubadilishana wahadhiri kutoka chuo kimoja kwenda kingine kwa makubaliano maalum na kufanya tafiti mbalimbali Ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango, ambapo hivi sasa wanaweza kufanya mikutano mingi mikubwa.
Profesa Kihampa amesema, kongamano hilo la 14 wa mtandao huo kwa kuwa ulikuwa ukifanyika nchi mbalimbali na Tanzania wamekuwa wakihudhuria kwa kuwa ni muhimu kwani wanashirikiana na wathibiti ubora kuanzia elimu ya msingi hadi ya juu.

Alisema kuwepo kwa mtandao mkubwa kuna vigezo vya uthibiti ubora walivyokubaliana vikiwemo sifa za mwalimu ziweje, mhitimu, elimu ya eneo fulani iweje na inasaidia kupata ajira sehemu yoyote duniani.


 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda akifungua kongamano la wadhibiti Ubora wa Elimu ya juu Barani Afrika (AfriQAN) Lililoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) nchini kwa ushirikiano na AfriQAN

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...