Na Mwandishi Wetu

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka imefanikiwa kupata faida shilingi bilioni 4.88 kabla ya kodi ikiwa ni ongezeka la asilimia 28 ikilinganishwa na kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022 ambapo faida ilikuwa shilingi bilioni 3.81.

Ongezeko hilo la faida limetokana na jitihada za kukuza mapato ya riba ambapo TADB imefanikiwa pia kiutendaji kukuza faida ya mapato ya riba (Net Interest Income) kwa kiwango cha asilimia 26% kutoka kipindi cha mwaka uliopita, kutoka shilingi bilioni 8.66 mpaka bilioni 10.94 katika robo ya tatu ya mwaka 2023.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Dkt. Kaanaeli Nnko alisema ukuaji huo wa mapato ya riba umechagizwa kwa kiasi kikubwa na ukuaji mikopo ya wakulima nchini hususani kwa wakulima wa mahindi, ngano, katani, pamba, kahawa, uvuvi, nyama, parachichi, korosho, maziwa, pilipili, zabibu, mpunga na alizeti, ambayo imenufaisha mikoa ishirini na saba (27) na wilaya mia moja na ishirini na nne (124).

“Kwa upande wa mapato yasiyokuwa ya riba (Non-Interest Income), TADB imefanikiwa kupata matokeo chanya kwa kuongezeka kwa asilimia 18% hivyo kufikia kiwango cha shilingi bilioni 1.52 katika robo ya tatu ya mwaka 2023. Mafanikio haya ni moja ya juhudi za kutoa mikopo na kuhakikisha inawafikia wakulima wengi nchi nzima.

“Kwa kipindi cha mwaka husika, mpaka TADB imefanikiwa kupata faida kabla ya kodi kiasi cha shilingi bilioni 12.34 ikiwa ni matokeo chanya na makubwa kiutendaji, vivyo hivyo ukuaji wa utoaji wa mikopo umekua kwa kiwango cha asilimia thelathini na sita na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 358.56. Katika kuendelea kuhakikisha ukuaji wa faida, taasisi itaendelea kuweka msisitizo na jitihada katika kuhakikisha inaendelea kuchagiza sekta ya kilimo nchini kama dira kuu ya utendaji wake,” alisema.

Katika hatua nyingine TADB imefanikiwa kupunguza uwiano wa kiwango cha mikopo chechefu kuwa chini ya kiwango kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) cha chini ya asilima 5 kwani katika kipindi husika kiwango kimekuwa asilimia 4.58 ukipungua kutoka asilimia 5.47 katika robo ya tatu ya mwaka jana.

Mafanikio haya ni muendelezo thabiti uliowekwa kuhakikisha ukuaji wa mikopo unaakisi kiwango cha chini cha mikopo chechefu ili kuhakikisha ustahimilivu na ukuaji wa taasisi.

Kwa ujumla mali za benki (Total Assets) zimeongezeka hadi shilingi bilioni 535.25. Ukuaji huu unatokana na Ukuaji wa mikopo katika sekta ya Kilimo Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Afia Sigge, alisema katika robo ya tatu ya mwaka (Q3) ya mwaka 2023, jumla ya Shilingi 61,883,235,022 zilitolewa kama mikopo katika sekta ya mazao, mifugo na uvuvi nchini.

"Kati ya shilingi bilioni 61 zilizotolewa kwa wakulima, Shilingi 40,236,677,059.00 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na gharama za uendeshaji wa shughuli za kilimo. Shilingi 19,236,098,697 zilikopeshwa kwa ajili ya gharama za ujenzi wa miradi ya kilimo. Shilingi 1,219,430,145 zilikopeshwa katika miradi ya umwagiliaji. Huku kiasi cha Shilingi 1,191,029,121 zikiwa zimekopeshwa katika ununuzi wa mifugo, nyenzo za kisasa za kilimo na ujenzi wa maghala.

Aidha, Meneja wa Mifuko ya Wakala kutoka TADB, George Nyamrunda alisema kwamba TADB inaendelea kufanya jitihada mahususi kwa ajili ya kuendeleza wakulima wadogo nchini kupitia Mfuko wa Udhamini wa Wakulima Wadogo (SCGS), kwa kutoa udhamini kwa wakulima wadogo ambao wanapata changamoto ya dhamana.

“TADB inashirikiana na taasisi kumi na sita za kibenki kupitia mfuko wa SCGS, Mpaka robo tatu ya mwaka huu, TADB imefanikiwa kudhamini jumla ya shilingi bilioni 228.26 kwa wakulima wadogo katika mikoa 27, na wilaya 127 nchini.


Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Dkt. Kaanael Nnko (wa pili kulia) akiongea wakati ya kutangaza taarifa za fedha za benki hiyo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka ambapo benki hiyo imepata faida ya shilingi bilioni 4.88 kabla ya kodi. Kulia ni Afia Sigge, kaimu mkurugenzi wa mikopo na biashara wa TADB. Wa kwanza kushoto ni Amani Nkurlu, Meneja Masoko na Mawasiliano akifuatiwa na George Nyamrunda ambaye ni Meneja wa Mifuko ya Wakala




Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dkt. Kaanael Nnko (katikati) akiongea wakati wa kutangaza taarifa za fedha za benki hiyo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka ambapo benki hiyo imepata faida ya shilingi bilioni 4.88 kabla ya kodi. Kulia ni Afia Sigge, kaimu mkurugenzi wa mikopo na biashara wa TADB na kushoto ni George Nyamrunda ambaye ni Meneja wa Mifuko ya Wakala


Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutangaza taarifa za fedha za benki hiyo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka ambapo benki hiyo imepata faida ya shilingi bilioni 4.88 kabla ya kodi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...