NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,imebaini miradi 27 ya sh.bilioni 8.165 kati ya miradi 35 ya maendeleo katika wilaya za Nyamagana,Magu,Misungwi na Ilemela imejengwa chini ya kiwango.
Akitoa taarifa utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humu,James Ruge,amesema leo kuwa, walifuatilia na kukagua utekelezaji wa miradi 35 ya maendeleo ya sh.bilioni 13.932, kufahamu ubora na thamani ya fedha iliyotumika.
Ruge amesema baada ya ukaguzi huo taasisi hiyo imeanzisha uchunguzi katika miradi iliyokutwa na mapungufu makubwa na yenye mapungufu madogo ikiwemo kuchelewa kukamilika walishauri yarekebishwe ili thamani ya fedha ionekane.
“Katika hiyo miradi 35 ya sekta za afya,barabara,elimu na utawala iliyofuatiliwa na kukaguliwa,miradi 27 ya sh.8,165,465,816.24 ilikutwa na mapungufu mbalimbali.Baadhi imejengwa chini ya viwango,matumizi ya vifaa duni visivyokidhi ubora na vifaa vingine vilichepushwa,”amesema.
Ruge amefafanua kuwa miradi ya Jiji (Nyamagana) iliyokutwa na kasoro ina thamani ya sh.bilioni 2.68 ambayo ni ujenzi wa jengo la ghorofa la Mirongo sekondari,barabara za Isamilo International,Nyehunge, Mahina,Ofisi ya kta Mabatini na shule mpya ya Kanenwa.
Kwamba Wilaya ya Magu inayotekeleza miradi ya sh. bilioni 2.576 walibainika kasoro katika ujenzi wa wodi ya kujifungulia,stoo ya dawa na wodi ya wanaume ya Hospitali ya Magu,jengo la wagonjwa wa nje la zahanati ya Busalanga,shule mpya za msingi Chief Hangaya na Kisesa,vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi Wita,Kanyama,Ilungu,Salisima na Bugomba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo miradi ya Wilaya ya Misungwi yenye thamani ya sh.bilioni 2.143 pia ilikuwa na kasoro katika ujenzi wa shule ya Sekondari Mwambola ambapo yalitumika matofali ya chini ya kiwango,bei ya vifaa vya ujenzi wa shule ya msingi Mwabebeya ilitofautiana na bei halisi,viti na meza za wanafunzi wa shule ya msingi Mwagiligili vilitengenezwa chini ya kiwango.
“Tumeanzisha uchunguzi wa miradi ya ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Nyabiti.Pia,unafanyika katika ujenzi wa barabara ya Fella-Ngereka-Nyashishi ambapo mitaro imeanza kubomoka na hivyo wakandarasi wa miradi hiyo wanatakiwa kufanya marekebisho,”amesema Ruge.
Pia katika kipindi cha Julai hadi Septemba taasisi imechambua mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi ya zuio na kubaini baadhi ya halmashauri hazikusanyi kodi hiyo,uelewa mdogo wa wafanyabiashara na watoa huduma wakiwemo mafundi ujenzi (Local) kutokuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN Number).
Ruge amesema kodi hiyo haikatwi moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara hao wanapofanyiwa malipo ya kazi zao,kutokana na mifumo ya halmashauri kutosomana na mifumo ya TRA,hivyo wanatarajia kukutana na wadau husika ili kuwapa matokeo ya kazi hiyo waliyoifanya na kuweka maazimio ya namna bora ya kukusanya kodi ya zuio.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo katika eneo la elimu kwa umma kwa kipindi hicho cha miezi mitatu iliyopita imefanya semina 70,mikutano ya hadhara 41,uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 101 katika shule za msingi,sekondari na vyuo,habari tisa zenye ujumbe wa kuelimisha na kukemea vitendo vya rushwa ziliandikwa,vipindi vitano vya redio na maonesho 10.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...