Meneja Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Valeria Milinga akizungumza na waandishi wa habari (Hawaii Pichani) mara baada ya ufunguzi wa kongamano la Kisayansi la Magonjwa yasiyoambukiza lililofanyika leo Novemba Mosi, 2023 jijini Dar es Salaam
Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya, Muhimbili(MUHAS) Prof Apolinary Kamuhabwa (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kingamano la kimataifa la kisayansi kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Novemba Mosi, 2023
Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa kisukari Tanzania na pia Mwenyekiti wa shirikisho la magonjwa yasioambukiza Profesa Andrew Swai, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kingamano la kimataifa la kisayansi kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Novemba Mosi, 2023.
Na Karama Kenyunko Michuzi tv
MENEJA Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Valeria Milinga amesema takwimu za magonjwa yasiyoambukiza zinaongezeka kwa asilimia 9.4 ikilinganishwa na miaka mitano ya nyuma.
Amesema kuanzia mwaka 2017 hadi 2021, watu waliofika hospitali na kugundulika na magonjwa yasiyoambukiza walikuwa milioni 2.5 na mwaka 2021 pekee waliofika vituo vya afya ni milioni 3.8 hivyo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 9.4.
Akizungumza katika kongamano la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza leo Dar es Salaam, Milinga amesema katika mpango huo unasimamia magonjwa yote yasiyoambukiza kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Afya.
"Tunafurahi tunawagundua mapema lakini pia tuna jukumu kubwa la kuongeza utambuzi wa wananchi mapema ili waweze kupata huduma stahiki, kuzuia madhara yanayoweza kutokea. Tumewekeza katika huduma za uelimishaji jamii na kuchunguza afya mapema kupitia majukwaa mbalimbali," amefafanua Milinga.
Pia amesema wana utaratibu wa upimaji wa afya mahala pa kazi na tayari Wizara 18 na wananchi 3,900 wamefikiwa.
Ametoa wito kwa watendaji wote kufanya upimaji huo katika maeneo ya kazi kupitia ofisi zilizopo na kutenga fedha kupima afya za wafanyakazi kwa sababu wako katika hatari kwani wanakaa muda mrefu, kutofanya mazoezi na kuzingatia ulaji unaofaa.
Amesema katika mpango huo wanaongozwa na mkakati wa Taifa wa III wa mwaka 2021 hadi 2026 na kwamba kuna maeneo mbalimbali ambayo wanategemea kuyaboresha ikiwemo usimamizi na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Sekta za Elimu, Ujenzi na Fedha wanashirikiana kudhibiti magonjwa hayo.
"Eneo lingine ni kuzuia na kuongeza uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kupima magonjwa hayo na kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza. Tunatoa elimu kwa jamii kuhusu mtindo wa maisha kwa kuhamasisha ulaji unaofaa, mazoezi na uthibiti wa matumizi ya sigara na dawa za kulevya," amesema.
Katika eneo la nne wanaboresha utafiti, takwimu na upatikanaji wa takwimu kwa urahisi ili kuleta taarifa juu ya magonjwa yasiyoambukiza.
"Katika kongamano hili, tutajadiliana kwa pamoja namna ya kuwekeza na kudhibiti magonjwa haya. Nimri inafanya tafiti wa Step ambao utatuonesha kwa ukubwa namna tulivyopiga hatua kuhusu viashiria vya magonjwa ikiwemo ulaji wa mboga mboga na matunda pamoja na matumizi ya tumbaku," amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema Amesema kuwa kongamano hilo ni la tano ambalo linalenga kujadili magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tatizo kubwa duniani kwani idadi ya watu wanaopata magonjwa hayo wanaongezeka.
Amesema katika mkutano huo kuna watafiti mbalimbali, watunga sera, watoa huduma na wagonjwa.
"Magonjwa ya kisukari, moyo, shinikizo la damu na saratani yameongezeka hivyo, watafiti waliopo watatoa matokeo ya tafiti zao ili tuyapitie na kuyajadili kisha tutoe mapendekezo yanapokwenda kwa watunga sera kuwa na mikakati ya pamoja," amesema Profesa Kamuhabwa.
Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuzuia kuongezeka kwa magonjwa hayo na hivyo waendelee kuwekeza katika kukinga kwani asilimia 60 ya watu wanaopata magonjwa hayo ni vijana.
Pia amesema magonjwa yasiyoambukiza nchini ndio yanazidi kuongezeka na kwamba chanzo kikubwa ni maisha wanayoishi na vyakula wanavyokula hivyo, elimu inahitajika.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa yasiyoambukiza, Profesa Andrew Swai lengo kusaidia watu waelewe tatizo hilo ili waweze kujizuia dhidi ya magonjwa hayo.
Swai amesema mwaka 1986 walifanya utafiti kwa watu 10,000 kutoka Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mara na kubaini asilimia moja ya watanzania ndio wana uelewa kuhusu ugonjwa wa kisukari.
Ameeleza kuwa asilimia tano ya watu hao ndio walikuwa na uelewa kuhusu ugonjwa wa shinikizo la damu na unene ni asilimia tano.
"Katika utafiti uliofanyika mwaka 2022, asilimia tisa ni ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu ni asilimia 26, unene ni asilimia 34. Tiba za magonjwa haya ni ghali kwani unapotaka kutibu. Kati ya wagonjwa 100 wa kisukari ni watu wawili tu wenye uelewa kuhusu ugonjwa huo," amesema.
Ameongeza kuwa kati ya wagonjwa 100 ni watatu tu ndio wanauelewa kuhusu ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hivyo kufikia hospitali wakiwa katika hali mbaya.
"Asilimia 20 ya bajeti yote ndio ingeweza kutibu magonjwa haya mawili ya kisukari na presha bila kuongeza saratani, moyo na mapafu,"
Pia amesema pamoja na mapendekezo ya bima ya afya kwa wote, bado hawataweza kumudu kuyatibu kwa kuwa Tanzania inatumia Dola 40 kwa mtu kwa mwaka wakati mataifa mengine wakitumia hadi Dola 4,000 kwa mtu mmoja.
Ameshauri jamii kuacha tabia bwete na ulaji usiofaa kwani ndio huchangia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza na kwamba wakiwahi mapema kugundua wanaweza kujirekebisha na kuondoka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...