Na Mwandishi wetu - Songwe

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasimu Majaliwa Majaliwa amesema Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini huku akitoa pongezi nyingi kwa Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo, Tarehe 24 Novemba wakati akiongoza hafla ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Ivugula, kata ya Mahenje katika Halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo katika kijiji hicho jumla ya shilingi milioni 207 zimetumika kufikisha nishati ya umeme huku bilioni 122 zikitumika kutekeleza miradi mitano (5) kwa mkoa wote wa Songwe.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kufikisha huduma mbalimbali katika maeneo ya vijiji ikiwemo nishati ya umeme wa uhakika na kusisitiza kuwa umeme ukitumika ipaswavyo; utasaidia kuinua uchumi wa Watu wengi ambao wengi wao, wanaishi vijijini.

“Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupa sisi (Mawaziri) pamoja na Watu wa REA agizo la kupeleka Wakandarasi vijijini, wapeleke nguzo na nyaya ili wafikishe umeme kwa Wananchi wa vijijini na Mhe. Rais amesema tunapoleka umeme, tusiangalie aina za nyumba, iwe ni nyumba ya ghorofa peleka umeme nyumba ya nyasi na udongo peleka umeme na Wananchi wa vijijini waunganishiwe kwa gharama nafuu ya shilingi elfu ishirini na saba (27,000/=)”. Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya utekerezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini katika Mkoa wa Songwe; Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti, Mhandisi, Godfrey Chibulunje amesema Serikali imetenga bilioni 122.7 kwa ajili ya utekerezaji wa miradi mitano ya kusambaza umeme katika vijiji na vitogoji vya mkoa wa Songwe.

Mhandisi Chibulunje ameitaja Miradi hiyo mitano (5) inayotekelezwa katika mkoa wa Songwe kuwa ni pamoja na Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II); Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B (REDPIIB); Mradi wa Kupeleka umeme katika Vitongoji (HEP); Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo; na Mradi wa tano ni wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

“Mkoa wa Songwe una jumla ya vijiji 307 ambapo hadi sasa vijiji 281 sawa na asilimia 91.5% vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini”. Amekaririwa Mhandisi Chibulunje.

Aidha; Mhandisi Chibulunje amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme vijijini nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa.

Naye Afisa Mpimaji Mwandamizi wa REA; Bwana Hussein Shamdas amesema Wakala upo katika hatua za mwisho katika kukamilisha mfumo wa taarifa wa kijiografia utakao kuwa ukitoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini na vitongoji.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...