Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Uongozi bora na imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unaendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya mataifa mengi duniani ikiwemo taifa la Urusi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye Kongamano la Kimataifa la Watu waliosoma nchini, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kutokana na uhusiano mzuri na Urusi, hivi karibuni Tanzania itasaini mikataba na taifa la Urusi kuhusiana na masuala ya kulinda amani, ulinzi na usalama pamoja na kudhibiti uhalifu.
“Tutaingia mikataba na taifa la Urusi, mikataba ya kubadilishana uhalifu, tutahakikisha hakuna uhalifu kwenye mataifa haya, wapo watu wanafanya uhalifu kwenye nchi moja na wanakimbilia kwenye nchi nyingine, tunaingia mikataba hii ili kuwakamata Wahalifu hao,” amesema Balozi Dkt. Chana.
Balozi Dkt. Chana ametoa wito kwa Watanzania kuwa nchi yao inaendelea kuwa na amani na utulivu, huku akibainisha kuwa Tanzania haitaruhusu kuwa uhalifu wowote. Pia amesisitiza watu kuendelea kuishi kwa amani na utulivu.
Tanzania imetumia fursa kwenye Kongamano hilo kutangaza vivutio vya uwekezaji ili wawekezaji mbalimbali waje kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Dkt. Binilith Mahenge amesema Tanzania ina sehemu nyingi za wageni kuwekeza.
Kwa upande wao baadhi ya Wahitimu wa Vyuo Vikuu nchini Urusi wamesema elimu walioipata nchini humo imewasaidia kuendeleza na kupambanua nchi ya Tanzania ikiwa pia kuwasaidia Wahitimu wa Vyuo vya hapa nchini.
“Nilipokuwa Kiwanda cha Urafiki tuliweza kutengeneza Mitambo mipya na mizuri iliyotoka nchini China, elimu niliyopata Urusi pia imesaidia kuwapa ujuzi Wanavyuo wa Chuo cha Maji na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT),” amesema Mhitimu wa mwaka 1991 katika Fani ya Uhandisi Mitambo (Mechanical Engineering),” Dkt. Dkt. Yona Kimori.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la Watu waliosoma nchini Urusi, Kongamano hilo limefanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Dkt. Binilith Mahenge akizungumza kwenye Kongamano hilo. Dkt. Mahenge ni mmoja wa Wahitimu wa Vyuo Vikuu nchini Urusi.
Sehemu ya Wataalamu mbalimbali na baadhi ya Wasomi waliosoma nchini Urusi wakiwa kwenye Kongamano hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...