Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema ziara iliyofanywa na Rais wa Romania Klaus Iohannis nchini imeendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili huku akieleza katika mazungumzo yao wamekubaliana kushirkiana katika masuala mbalimbali yakiwemo ya dawa na usindikaji kwa mazao ya kilimo.
Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Rais Dk.Samia amesema kwa niaba ya wananchi wa Tanzania wanayofuraha kubwa ya kumpokea Rais na ujumbe wake na kwamba utaendelea kudumisha ushirikiano.
“Uhusiano wetu ulainza Mei mwaka 1964 ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hivyo Romania ni mbia wetu na ni muhimu kuendelea kuimarisha uhusiano huu. Na hili limethibitishwa na makubaliano ambayo tumesaini leo,” amesema.
“Tumekubalia kuchukua hatua za pamoja kuendelea kuimarisha zaidi sekta mbalimbali kama sekta ya dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini pamoja na kukabiliana na majanga.Pia tumekubaliana ufadhili wa masomo katika udaktari na famasia," ameongeza.
Rais Samia amesema katika mazungumzo hayo, Romania imekubali kutoa nafasi 10 za Watanzania kwenda kusoma kwa masomo ambayo watachagua, huku Tanzania ikitoa nafasi tano za ufadhilii kwa wanafunzi wa tano wa Romania kuja kusoma nchini.
“Katika mazungumzo yetu pia tumezungumza kuhusu kuimarisha sekta ya biashara hasa kukuza zaidi biashara kwa kuangalia maeneo ambayo tunaweza kufanya pamoja, kualika wafanyabiashara wa Romania kuja Tanzania na Watanzania kwenda Romania kubadilisha uzoefu.
Amesema wamekubaliana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zao kuendelea kuzungumza mara kwa mara, ili kuhakikisha fursa zilizopo baina yao zinatumika ipasavyo kwa maslahi ya pande zote.
Aidha, Rais Dk.Samia ameipongeza Romania kukubali kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Pia amesema wameomba Romania isaidie kuwapa nguvu katika kuhakikisha Tanzania inafanikiwa katika eneo la nishati safi ambayo inahitaji kwa matumizi mbalimbali kwa sasa.
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema wakati umefika kwa kuanza utekelezaji wa makubaliano waliyosaini mwaka 2018, kuhusu kufanya mikutano ya mazungumzo ya kisiasa.
Amesisitiza ni matumaini yote ambayo wameyazungumza yatatekelezwa kwa maslahi ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake Rais Iohannis amesema mwakani Romania na Tanzania zinatumika miaka 60, hivyo kupitia ziara hiyo wamejadiliana namna ya kuboresha na kuendeleza mazuri ambayo yamefanyika.
Amesema mikakati yao ya kurejesha ushirikiano na nchi za Afrika utahakikisha Tanzania inanufaika zaidi.
Rais Iohannis amesema sekta ya kilimo na majanga itapewa msukumo mkubwa kwani zina mchango kwenye maendeleo.
"Tunatamani sekta ambazo tumekubaliana zinafanikiwa kwa kasi ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana. Mfano sekta ya ulinzi, teknolojia na usalama wa mitandaoni,"amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Romania Mhe. Klaus Iohannis wakati wakishuhudia utiaji saini wa Mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo iliyotiwa saini na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda na Waziri wa nchi wa masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian- Laurentiu Hristea kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Novemba 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Romania Mhe. Klaus Iohannis wakati wakishuhudia utiaji saini wa Mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini tarehe 17 Novemba 2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...