NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MFUKO
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeshalipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 65.4
hadi kufikia Septemba, 2023.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, wakati akitoa
wasilisho lake katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari, kuelezea
utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya WCF, miaka 8 tangu kuanzishwa kwake.
Sambamba
na hilo pia amesema Mfuko umeweza kusajili asilimia 95% ya waajiri wote
wanaostahili kujisajili na Mfuko na kuahidi kuwa Mfuko uko mbioni kukamilisha
asilimia 5% ya waajiri ambao bado hawajajisajili na Mfuko.
Mafanikio
mengine ameyataja kuwa ni pamoja na kupanuka kwa wigo wa utoaji huduma kwa
kuingia makubaliano na hospitali, watoa huduma mbalimbali za afya nchini na
ufunguzi wa ofisi mikoani.
Pia
aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kuboreshwa kwa huduma kupitia usimikaji
mifumo ya TEHAMA, kuboreshwa kwa kituo cha huduma kwa wateja (Call Centre) na
kuboreshwa kwa tathmini za ulemavu kupitia mafunzo kwa madaktari sehemu
mbalimbali nchini.
Akieleza
zaidi alisema, hadi kufikia Septemba 2023, thamani ya Mfuko imefikia bilioni
697.5
Alisema
jambo jema ni kwamba Mfuko kuwa na uwezo endelevu wa kulipa fidia mpaka mwaka
wa fedha 2047/2048 kulingana na tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko ya mwaka
2018, ambayo ilifanywa na Shirika la Kazi Duniani ILO.
“WCF
imefanya tathmini ya pili mwaka 2022 ambayo imeonesha kuwa Mfuko ni himilivu na
unauwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kutetereka.” Alisisitiza Dkt. Mduma.
Alisema
WCF sio tu inalinda nguvu kazi ya taifa lakini pia waajiri sasa wana muda mrefu
wa kuendelea na kazi za uzalishaji huku jukumu la kumuhudumia mfanyakazi
aliyeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi likibebwa na WCF.
“Lakini
pia uwepo wa WCF umeleta tija kazini kutokana na mahusiano mazuri kati ya
waajiri na waajiriwa, lakini pia kupunguza umaskini hususan kwa wategemezi na
wafanyakazi wanaopata ulemavu wa kudumu na kushindwa kurudi kazini au kufariki.”
Alisema.
Alisema
Mfuko unachangia ongezeko la uzalishaji na maendeleo ya Taifa kupitia ongezeko
la tija, ongezeko la pato la taifa na kodi ili kuiwezesha Serikali kuboresha
utoaji wa huduma kwa wananchi
Dkt.
Mduma pia alisema, kutokana na mafanikio ambayo Mfuko umeyapata, umekuwa kinara
na umeweza kuwafanya majirani toka nchi za Zambia, Kenya, Botswana, Afrika
Kusini na Zimbabwe kujifunza kutoka WCF.
Akizungumzia
majukumu ya WCF, Dkt. Mduma alisema, ni pamoja na Kusajili Waajiri waliopo
katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara, Kukusanya michango kutoka kwa
Waajiri, Kulipa Fidia kwa Mfanyakazi atakayeumia, kuugua ama kufariki wakati akitekeleza
majukumu ya mwajiri wake.
Majukumu
mengine alitaja kuwa ni Kutunza kumbukumbu za matukio ya ajali, magonjwa na
vifo kutokana na kazi, Kukuza mbinu za kuzuia ajali, magojwa na vifo kutokana
na kazi na Kuelimisha Umma kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Kwa
upande wake, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ambayo ndiyo yenye jukumu la
kusimamia utendaji wa Mashirika yote ya Umma, imeweka utaratibu kwa viongozi wa
taasisi hizo kukutana na wahariri na waandishi wa habari ili kuueleza umma wa
Watanzania mambo ambayo taasisi hizo zinatekeleza.
Chini
ya utaratibu huo WCF inakuwa ni taasisi ya 11 kukutana na wahariri na waandishi
wa habari nchini.
“Kwa
mantiki hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina ikaona umuhimu na msingi wa
kuzikutanisha taasisi za umma na umma wenyewe kupitia vyombo vya habari.”
Alisema Bw. Thobias Makoba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya
Msajili wa Hazina (TR)
Alisema,
malengo sio tu kutoa elimu lakini iwe ufunguo kwa taasisi kufanya muendelezo wa
kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Akifafanua
zaidi alisema, Msajili wa Hazina (TR) alielekeza mara kadhaa kwa taasisi za
umma kila zinapoandaa taarifa za fedha za kila mwaka wahakikishe zinatangazwa
ili umma ujue mwenendo wa mashirika yao.
"Umma
ukiwa na uelewa wa kutosha itakuwa rahisi kwao kubaini usahihi wa kinachoelezwa
kuhusu taasisi fulani." Alisema Bw. Makoba.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus
Balile, ameishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuandaa utaratibu wa wakuu
wa taasisi kukutana na vyombo vya habari.
“Lakini
hapa nataka niwaambie ninyi wahariri na hawa ndugu zetu wanaofaidika na fidia,
muwe mabalozi wa Mfuko huko muendako ili watanzania wengi zaidi waweze
kufaidika na huduma za WCF.” Alisema.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Fidida kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kushoto),
akiwasalimia wanufaika wa WCF wakati akiwasili kwenye kikao kazi na Wahariri wa
vyombo vya habari kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya WCF jijini Dar es Salaam
Novemba 2, 2023. Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR)
ili kutoa fursa kwa watendaji wa WCF kueleza utekelezaji wa majukumu na
mafanikio ya Mfuko huo miaka 8 tangu uanzishwe. Wanaofuatana na Dkt. Mduma ni
Bw. Thobias Makoba (watatu kushoto) ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
na Uhusiano, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Bw. Sabato Kosuri, Afisa Mwandamizi
wa Uhusiano Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...