ALIYEKUWA Mwanafunzi wa chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya, Yoakim Ndunguru amewatoa chozi mamia ya wananchi wakati jina lake likitajwa kutunukiwa cheti na mkuu wa chuo hicho, Dk Ali Mohamed Shein.

Ndunguru alikuwa anahitimu elimu yake ngazi ya Astashahada ya uhasibu ambaye imeelezwa amefariki dunia ikiwa ni siku chache kabla ya mahafari hayo wakati wa likizo baada ya kuumwa.

Akizungumza wakati wa mahafari ya 22 ya chuo hicho yaliyofanyika leo Novemba 30, makamu mkuu wa chuo, Prof. William Mwegoha amesema mwanafunzi huyo alikuwa amekamilisha kila kitu tayari kwa mahafari lakini hakuweza kufanya sherehe.

“Mkuu wa Chuo (Dk Shein) huyu mwanafunzi ni wa ngazi ya Astashahada kozi ya uhasibu ambaye alifariki dunia na alikuwa amekamilisha kila kitu tunaomba kipekee umtunuku cheti” amesema Mwegoha huku huzuni na simanzi zikitawala kwa wahitimu na wananchi waliojitokeza katika mahafari hayo.

Mwegoha ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi 1,295 wamehitimu mafunzo ya kozi mbalimbali na kwa ngazi tofauti huku akieleza kuwa mafanikio ni makubwa.

“Lakini tumeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi ikiwamo zahanati ya chuo utakaogharimu Sh 465 milioni, elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi unaofadhiriwa na benki ya dunia kama mkopo wa serikali,” amesema Profesa huyo.

Akifunga mahafari hayo, Dk Shein amewataka wahitimu kuendelea kujiongezea elimu ili kufungua milango zaidi ya fursa na kujiajiri akieleza kuwa kwa sasa wasomi ni wengi na idadi ya watu inaendelea kuongezeka kuliko ajira.

Amesema serikali imetimiza wajibu wake kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya chuo hicho na kwamba siku za mbeleni kitaweza kupiga hatua kufika anga za kimataifa.

“Haifai kukata tamaa, bali kujiamini na kujituma ndio siri ya maendeleo na dunia ya sasa inahitaji kupambana kwani ajira ni za kupambania hivyo jiongezeeni elimu ili kufungua milango mingine,"

“Fanyeni tafiti na kubuni teknolojia mpya ambazo zitaendana na wakati wa sasa, ajira zina ushindani na wasomi wanaongezeka, serikali imetimiza wajibu kwa kuweka miundobinu,” amesema Dk Shein.

Naye mwanafunzi bora wa chuo hicho, Rojas Mwalurefu amesema haikuwa kazi rahisi kumaliza masomo akieleza kuwa Mzumbe ni chuo bora ambacho kinaendelea kutayarisha viongozi wapya.

“Tunamshukuru Mungu aliyetujalia kumaliza masomo yetu, haikuwa kazi rahisi bali uvumilivu, nidhamu na kujituma kuyafikia mafanikio, chuo hiki kimeendelea kutoa wasomi wengi na tunajivunia,” amesema Mwalurefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...