Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kagera

ASKOFU wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dk.Benson Bagonza amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa ujasiri na wenye gharama za kisiasa baada ya kuamua kuingia katika mchakato wa kutafuta maridhiano katika makundi mbalimbali yakiwemo ya vyama vya siasa.

Dk.Bagonza ametoa pongezi hizo leo Desemba 10, 2023  wakati  wa Misa Maalum ya kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera leo Desemba 10,2O23, ambapo amesema Kanisa ni alama ya upatanisho.

“Kanisa ni moja ya alama ya upatanisho na moja ya R ya Rais wetu, Dk.Samia inamaanisha mariadhiano, yaani upatanisho.Napenda kumpongeza Rais wetu kwa ujasiri wenye gharama za kisiasa pale alipodiriki kuingia katika mchakato huo wa maridhiano.

“Mama ni jasiri na  sina mashaka naye. Upatanisho mahali popote una baraka za Mungu , na anayesita au kuvuruga upatanisho anafarakana na Mungu. Napenda kumshukuru Rais kwanza kwa kuniamini na kunishirikisha katika jitihada hizo za maridhiano.

“Kupitia hekalu hili napenda kumtia moyo , na naomba mumpelekee ujumbe wangu asiache kushughulikia maridhiano katika Taifa letu kwasababu kuridhiana ndio afya ya taifa letu, na katika maridhiano aliangalia makundi mbalimbali.

“Kuna makundi mbalimbali hasidi hayakai katika amani wakati wote.Kuna walipa kodi na watoza kodi ambao hawapati siku zote , kuna wafugaji na wakulima , kuna vyama vya siasa na chama tawala , kuna wanaharakati na Serikali,”amesema Askofu Dk.Bangoza.

Ameongeza pia kuna kundi la madereva na wamiliki, kuna bodaboda na polisi, kuna machinga na halmashauri , kuna Serikali na vijana wasio na ajira.“Makundi yote haya yanahitaji maridhiano na upatinisho.”

Amefafanua  kundi pekee lisilohitaji upatanisho ni la viongozi wa dini na shetani, lakini katika maisha ya siasa usipopatana na mpinzani wako basi ujifunze kuishi naye bila kumaliza na bila kuruhusu yeye kukumaliza, hiyo ndio siasa.

Wakati huo huo Askofu Bagonza amezungumzia tatizo la ajira nchini ambapo amesema  pamoja na jitihada kubwa za Serikali katika eneo hili kuna mambo mawili lazima kuyakubali hata kama yanaumiza na yanagharama kisiasa.

Amesema jambo la kwanza,  Serikali haina uwezo wa kuajiri wahitimu wote nchini , Serikali yenye uwezo huo haipo duniani kokote."Najua hili linauma lakini lazima tukubali ukweli.

Pia amesema elimu yetu inaanda watu kuajiriwa badaa ya kujiajiri kwa hiyo wanaotafuta kazi wasibezwe siwabeze maana ndicho waliochoendea shule."Sasa kutokana na ukweli huu mchungu napenda kuishauri Serikali mambo mawili.

"Serikali itengeneze sera rafiki , kuiwezesha sekta binafsi, muwekezaji na wadau wengine wa maendeleo ili kila muajiri apate nafuu ya namna fulani kumuwezesha kuajiri watu wengine zaidi,”amesema.

Ametoa mfano kila mwajiri anayeajiri watu zaidi ya 10, Serikali imsaidie kulipa asilimia 10 iende NSSF, kwa masharti kuwa alipe mshahara usio chini ya kima cha chini cha mshahara kilichokubaliwa kisheria.

Askofu Bagonza amesema vivutio vya namna hiyo kama msamaha wa kodi, au tozo kadhaa  pamoja na  nafuu zingine za waajiri zinaweza kumeza sehemu kubwa ya vijana wasio na ajira.

Amesema hivi sasa waajiri binafsi wanasita kuajiri kwasababu sheria zilizopo za ajira hazimuangalii anayeajiri zinamuangalia anayeajiriwa. “Kwa hiyo kwa hiyo kuliko nilete kero ya kupelekwa mahakamani, hapana kaeni huko nitafanya kazi mwenyewe na vijana wanazidi kuteseka bila ajira."

Amefafanua kwamba Sheria zinazozuia watu wasiajiriwe haziwasaidii wasio na ajira , hivyo kuna haja ya kuangalia suala hilo.

Ametoa ushauria  vyuo vikuu na vyuo vya kati vianzishe program maalum ya kuandaa wahitimu kufanya kazi wasizozisomea, na wafanye hivyo bila manung’uniko na vijana watakaoweza kujiajiriwa waandaliwe mpango maalumu wa kuwasaidia miaka ya mwanzo ili waimarike.


Pamoja na hayo Askofu Dk.Bagonza amesema kwa niaba ya dayosisi hiyo  anamshukuru Rais Samia kwa kuwa mmoja wa wachangiajia wa ujenzi wa Kanisa hilo.Mchango wake waliupokea na kwa upendo wake na unyenyekevu aliposikia wanachangishana wala hakumuomba  bali aliposikia alichangia.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu  Dk.Dotto Biteko amesema Rais Dk.Samia ni muumini namba moja wa maridhiano na upatanisho na ameyaishi kwa kuyatenda , tena wakati mwingine bila hata watu wa ndani ya Chama chake kumuelewa kwa urahisi .

“Akasema  nchi yetu hii ni yetu sote mwenye chama chake atabaki na chama chake, wewe wa CCM mpende wa upinzani, tuungane pamoja tusukume nchi yetu iende mbele.Hakuishia hapo akaunda na kamati ya pamoja , CCM wakaingia ndani , wapinzani wakaingia ndani…

“Na viongozi wa dini wakaingia ndani kwa maana moja tutafute muaka wa kitaifa tujenge Tanzania bora kwa ajili ya vizazi vinavyokuja.Amekuwa muumini si kwa kuigiza bali kwa dhati ya moyo wake mahali pengine waliozoea walikuwa wanatia mashaka."

ASKOFU wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dk.Benson Bagonza akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Abdulrahman Kinana wakati  wa Misa Maalum ya kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera leo Desemba 10,2O23





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...