Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Kampuni ya Franone Mining and Games limetd inayojishughulisha na uchimbaji madini ya vito ( Tanzanite) imeungana na watanzania wengine na Serikali katika kuchangia mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula Kwa waathirika wa mafuriko wilayani Simanjiro mkoani Manyara .
Akizungumza na waandishi na waandishi wa habari baada ya kutoa msaada huo, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Vitus Ndakize amesema wameguswa na tukio hilo hivyo wao kama wawekezaji waliowekeza kwenye uchimbaji wa madini wameona wachangie watanzania wenzao ambao wamepatwa na majanga hayo Kwa kutoa bidhaa mbalimbali pamoja na chakula.
Amesema miongoni mwa vitu ambavyo wamechangia na kukabidhi Kwa mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Seleman Selela ni pamoja na magunia 200 ya mahindi , maharagwe gunia 40 ,Sukari mifuko 20, na mafuta kantoni 40 za lita moja ambapo jumla ya msaada wote ugharama zote ni Sh.milioni 31.
Vitus ameongeza kuwa wao kama Kampuni wamekabidhi mahitaji hayo hivyo viongozi husika ndio wataona wanagawaje lakini wameelekeza kwenye kata mbili ambazo ni ,kata ya mto wa tembo , na kata ya shambalai.
" Kampuni tumetoa kwa ujumla ila uongozi wa Wilaya wao ndio wanajua namna watakavyogawanya chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo husika."
Pia Vitusi amewashauri wadau kuendelea kujitoa kwa hali na mali na kwamba wakati mwingine majanga kama hayo yanapotokea watu wanakuwa hawajajipanga, hivyo ni vema kujitoa kusaidia wenye uhitaji.
Ametoa mwito kwa watanzania kuendeleza umoja kama watanzania na hasa yanapotokea majanga kama hayo huku akiipongeza Serikali hasa ngazi ya Wilaya imefanya kazi kubwa kuhakikisha waathirika hao wanapata mahitaji ya kibinadamu.
"Na kwasababu Serikali haiwezi kufanya kila kitu kwa hiyo na sisi kama wadau tumeona tutoe mchango wetu ili kuunga mkono jitihada za Serikali kuhudumia watu wake."
Akimzungumzia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ukatisha ziara na kurudi haraka nchini kuungana na watanzania wengine baada ya kutokea mafuriko ya matope Hanang, Vitusi amesema Rais Dkt Samia ameendelea kuthibitisha yeye ni mtu wa watu na anawapenda wananchi.
Ameongeza Rais Dk.Samia ni mama anayejali watu wake na aliamua kukatisha ziara yake ya kikazi ili kuja nyumbani na kuwaona wananchi wake waliokumbwa na mafuriko hayo yaliyosababisha vifo , majeruhi na uharibifu wa mali.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Simanjiro mkoani Manyara Christopher Ole Sendeka ameipongeza kampuni ya Franone Mining and Games kwa kuwachangia waathirika wa mafuriko hayo.
Ole Sendeka amesema kampuni hiyo imekuwa msaada mkubwa kwenye jamii kwani hivi karibuni wakati wa ukame ilisaidia chakula kwenye shule mbili zilizokuwa zinakabiliwa na uhaba wa chakula zilizopo kata ya Naisinyai
Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Asia Ngaliwason ameishukuru kampuni hiyo na kuwahakikishia msaada huo utafika kwa wahusika waliokumbwa na mafuriko
Ameongeza kuwa waliokumbwa na mafuriko ni watu 126 na watapata msaada huo katika kata za shambarai na kata ya msitu wa Tembo kwenye kaya 49.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...