KAMPUNI ya Alliance One Tobacco Tanzania Limited (AOTTL) yenye makao makuu yake Morogoro, imetwaa tuzo kubwa ya viwanda vya kusindika tumbaku katika msimu wa 17 wa Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora (PMAYA) zilizoandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), ikiwapiku wazalishaji wengine wengi katika kipengele hicho.

Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi katika tuzo hizo zinazofanyika kila mwaka, akikabidhi zawadi kwa washindi jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Msemaji wa kampuni hiyo, Wakili John Magoti alipokea tuzo kwa niaba ya kampuni.

Akitoa maelezo ya kuhusu kampuni pembeni mwa PMAYA, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ephraim Mapoore, alisema Alliance One imeshinda tuzo hiyo si kwa bahati mbaya au bila kutarajiwa, bali ufanisi mkubwa wa kampuni hiyo katika kilimo bora na ufuasi wa taratibu za mikataba na wakulima iliyoingia nao kandarasi.

Kampuni ya Alliance One Tobacco Tanzania (AOTTL) imelipa jumla ya Dola za Marekani milioni 71.9 (Sh. bilioni 179.8) kwa wakulima zaidi ya 12,000 walioingia mkataba nayo wa tumbaku nchini msimu huu. 

Ni malipo yaliyolipwa kwa wakati, yaliyotokana na tumbaku yenye ubora wa juu.
Vilevile, kampuni imelipa Dola milioni 1.81 (Sh. bilioni 4.6) kwa ada za Vyama vya Ushirika vya Masoko ya Kilimo (AMCOS) kwa mwaka huu.

Kampuni pia imelipa Dola 780,000 (Sh. bilioni 1.95) kama ushuru kwa vyama vya ushirika vya tumbaku, ambavyo ni vyombo vikuu vya ushirika vilivyoanzishwa.
Pia imelipa jumla ya Dola za Marekani milioni 1.72 (Sh. bilioni 4.3) kama malipo ya mazao, kiasi ambacho kwa kawaida hulipwa moja kwa moja kwa wilaya mbalimbali inazofanyia kazi. 

Malipo haya yalifanywa kwa kuzingatia agizo la serikali la hivi karibuni kwamba malipo yote ya tumbaku kwa wakulima yanapaswa kufanywa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya kukamilika kwa mnada wa soko na malipo yote lazima yafanywe kwa Dola ya Marekani.

Kwa kawaida kampuni hutenga Sh. milioni 400, kila mwaka kwa ajili ya kurudisha sehemu ya faida kwa jamii inayozunguka maeneo ya shughuli zake, ikichangia katika miradi ya maji, afya na elimu.

Mwaka huu kampuni imetoa vifaa vya shule vyenye thamani ya Sh. milioni 222.762 kwa shule mbili za msingi za Morogoro ambazo ni Kingolwira na Bungo. 

Msaada huo uliowanufaisha moja kwa moja jumla ya wanafunzi 3600 katika shule zote mbili, ulitumika katika ujenzi wa madarasa na vyoo.

Ni kwa mwaka huu pia kampuni hiyo imetoa kompyuta tatu za kisasa na vifaa vingine vya kisasa vyenye thamani ya milioni 8.8 kwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro kusaidia kufanya upasuaji wa mifupa. 

Kadhalika, kampuni imetoa msaada wa kompyuta kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupambana na uhalifu.

Kampuni hiyo pia imetekeleza miradi ya upandaji miti katika wilaya tatu za Mkoa wa Kigoma, jumla ya ekari 1412.5 zimepandwa na kusimamiwa tangu mwaka 2014.

Kampuni hiyo ilipanda miti kwa kushirikiana na wakulima walioingia nao ubia katika wilaya tatu za mkoa huo ambazo ni Uvinza, Buhigwe na Kasulu.

Kampuni hiyo pia mwaka huu imezindua eneo la Ngukumo wilayani Nzega kwa ajili ya usambazaji wa kuni endelevu kwa wakulima wake wa tumbaku walioingia mkataba wenye jumla ya hekta zaidi ya 7,000 chini ya usimamizi wa pamoja wa misitu.
Alliance One ilifungua kiwanda chake cha usindikaji mnamo 1998 na imekuwa inafanya kazi kwa mafanikio tangu wakati huo bila kukosa msimu wowote wa mazao na kwa sasa ina wafanyikazi 350 wa kudumu na wanaolipwa pensheni pamoja na wafanyakazi wa msimu 3,000 kila mwaka.Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Mh.Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Msemaji wa Kampuni ya tumbaku Alliance One Wakili John Magoti, tuzo ya ushindi wa mzalishaji mkubwa sekta ya viwanda vya tumbaku nchini katika hafla ya tuzo za Rais kwa wazalishaji bora zinazoandaliwa na CTI.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...