Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kagera.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana ni muhimu kwa wananchi wa Kagera kuungana kuhakikisha mkoa huo unakuwa na maendeleo kama ambavyo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekusudia kuyafanya mkoani humo.

Adha, amesisitiza kuwa maendeleo katika eneo lolote huambata na changamoto yakiwemo machungu, hivyo wananchi wawe tayari kuvumilia, kushirikiana na kuacha malumbano yanayowakwamisha kuvuka kutoka eneo moja kwenda lingine.

Kinana ameyasema hayo leo Desemba 11, 2023 Bukoba mkoani Kagera alipozungumza na wazee wa mkoa huo ambapo amesema kufanikiwa kwa mkoa huo kunatokana na utashi, utayari na uchapa kazi wenye tija kwa maslahi ya wananchi wengi.

Makamu Mwenyekiti Kinana ameeleza kuwa mkoani Kagera serikali inatekeleza miradi mikubwa minne ukiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne, soko la kisasa katika Mji wa Bukoba na stendi ya mabasi mabasi ya mikoani.

“Hapa (Bukoba) mna bandari inajengwa kwa sh. bilioni 39, bandari hii itakuwa inaungana na reli ya mwendo kasi (SGR), reli ikitoka bandari inakuja moja kwa moja hadi Mwanza, ikifika Mwanza inakwenda hadi bandarini Mwanza, inakuja na mabehewa ya Uganda…yanapandishwa kwa njia ya reli na juzi Waziri wa Uchukuzi (Profesa Makame Mbarawa) amesema watu binafsi wataruhusiwa kununua mabehewa watatumia hiyo reli na watalipa.

“Ninyi mnajengewa barabara nne kwa sababu kila mji Tanzania una barabara nne, Arusha inatoka mjini hadi Tengeru, Mbeya barabara nne inajengwa, Songea inajengwa, Moshi (Kilimanjaro) inajengwa kwa nini ninyi hamtaki ijengwe. Kwa sababu kuna watu wachache hawataki ijengwe kwa maslahi yao binafsi,” amesema.

Kwa mujibu wa Kinana, kuna baadhi ya watu wanahoji ni kwa nini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anasifiwa, lakini jibu lake ni kwamba anapewa sifa kutokana na kazi nzuri anayoifanya.

Akifafanua zaidi kuhusu juhudi za maendeleo zilizofanywa na Rais Samia, Kinana ametumia fursa hiyo kupongeza uzinduzi wa mchakato wa kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 ambapo amesema ni jambo jema kwa kuwa inabeba maendeleo ya taifa.

Kielezea zaidi Kinana amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imezidi kuleta matumaini ya kufungua maendeleo kwa kuwa ina miradi ambayo inawagusa wananchi.

“Ukiangalia miradi ya maji, elimu, miundombinu pamoja na mingineyo ya kimkakati hakuna mradi ambao utekelezaji wake uko chini ya asilimia 80,” ameeleza.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara,  Abdulrahman Kinana ametembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa stendi ya kisasa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera leo Desemba 11,  2023.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana akisalimiana na Wananchi pamoja na Wafanyabiashara katika Soko la Bukoba linalotarajiwa kujengwa upya katika manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera, leo Desemba  11, 2023.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...