Bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imewahakikishia wanachama wake usalama wa fedha zao na kutaja kuwa zitarejea kwa wakati kutokana na kukamilika kwa kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho sasa kimeanza uzalishaji wa awali wa sukari ili kuondoa changamoto ya uagizwaji wa sukari kutoka nje ya Nchi.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika Kiwanda hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Mwamini Malemi alisema kuwa wamefurahi kutekeleza maagizo ya Serikali ambayo yaliwezeshwa kujengwa kwa kiwanda hicho na kuanza kwa uzalishaji.

Alisema wamefurahi kama NSSF pia kuona kwamba kiwanda hicho ambacho mpaka sasa kimeajiri wafanyakazi 5,000, kinakuwa na mchango mkubwa katika ajira na uzalishaji wa sukari ambao unakwenda kuunga jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la ajira kwa vijana.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hodhi ya Mkulazi, Dk Hilderither Msita alisema wamefurahishwa na hatua za Bodi ya wadhamini ya NSSF kutembelea kiwanda hicho kuona maendeleo ya ujenzi wake pamoja na hatua za mwisho za ujenzi zilizofikiwa.

Alisema kuwa majaribio ya mitambo ya kiwanda hicho kipya yamekamilika kwa ufanisi mkubwa na sasa Watanzania wakae mkao wa kula kwani bidhaa zake zitaingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa.

Alisema pamoja na kutengeneza sukari kwa matumizi ya majumbani pia kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza sukari ya viwandani.

Kwaupande wake Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Selestine Some aliishukuru Serikali kwa kazi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na maelekezo yake katika miradi ya kimkakati iliyowezesha kiwanda hicho kujengwa na kuanza kwa uzalishaji.

Kiwanda hicho chenye mitambo ya kisasa kinatarajiwa kwenda kuzalisha Sukari Tani 50, 000 hadi 75, 000 kwa mwaka, Huku kikiwa na uwezo wa kufua umeme Megawati 15 ambapo Megawati 8 zikitumika katika shughuli za kuendesha mitambo, na Megawati 7 zikirudi katika Gridi ya Taifa.



Meneja wa Mashamba ya Miwa Mbigiri Mhandisi Flavian Reginald akitoa maelezo ya kina juu ya hatua za uandaaji wa mashamba mpaka kufikia hatua za uvunaji kwa Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) walipotembelea katika maeneo mbalimbali ya mashamba hayo.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...