Na Said Mwishehe,Michuzi TV

BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa zawadi za sikukuu ya Krismas na mwaka mpya yenye thamani ya sh. milioni 17 kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha Taifa cha Kulea Watoto Wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Kurasini, Dar es Salaam.

Akizungumza leo alipokuwa akikabidhi zawadi hizo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano MSD, Eti Kusiluka amesema katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismas na mwaka mpya bohari hiyo imeona haja ya kufurahi na watoto hao kwa kuwapelekea zawadi.

“Sisi ni wazazi na watoto hawa na wana haki ya kufurahia kwa hiyo tumekuja na dawa za miswaki 400, mchele kilo 300, maharagwe kilo 100, unga kilo 300, vifaa vya shule yakiwemo madaftari, kalamu, penseli, mafuta, sabuni za kufuli na kuogea na mafuta ya kupaka.

“Mbali na zawadi hizo tumekuja na bidhaa ambayo tumeitoa kwenye ghala letu la MSD ya magodoro 80. Hivyo zawadi zote za sikukuu pamoja na vifaa vya shule ambavyo tumekabidhi vinagharimu sh. milioni 17. MSD imetoa zawadi kwa watoto hawa wafurahie sikuu, tunatambua kuwa watoto hawa wanaohitaji furaha kama watoto wengine.”

Kwa upande wake Meneja wa  MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie Kaema amesema wamefika kwa watoto hao kufurahi nao kama wanavyofurahi na watoto wao walioko nyumbani.

“MSD tumeamua kuja kwa kufurahi na watoto hawa , na hii si mara ya kwanza kuja kuwaona, tumekuwa tukifanya hivyo mara kadhaa. Sisi ndio mama zao, ndio baba zao kwa hiyo tumekuja kuwapa kidogo tulichonacho ili furaha yao itimie.

Awali Ofisa Ustawi wa Jamii Kituo cha Taifa cha kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Kurasini Farida Ismail ametoa shukrani kwa MSD kwa kuwapatia zawadi hizo ambazo zinakwenda kusaidia katika malezi ya watoto hao.

Amefafanua msaada huo wa MSD unakwenda kunufaisha watoto wapatao 60 wanaolelewa katika kituo hicho huku akitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wadau wengine kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwemo ya vituo vinavyolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa TEHAMA na Takwimu kutoka MSDLeopold Shayo amesema wametoa msaada huo kama sehemu ya kutekeleza wajibu wa Serikali wa kusaidia wenye uhitaji wakiwemo watoto hao ambao wanalelewa katika kituo hicho.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...