Na Muhidin Amri,Mbinga


JUMLA ya vitambulisho 131,181 vya Uraia(NIDA),vimeanza kugawiwa kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,ambavyo vitasaidia kupunguza kero kwa wananchi wanapohitaji kupata baadhi ya huduma za kijamii na Serikali.

Kwa muda mrefu,wananchi wamekuwa wakitumia namba pekee za Nida badala ya vitambulisho, hali ambayo imekuwa ikisababisha baadhi yao kusahau namba hizo na kutopata huduma muhimu wanazohitaji.

Afisa usajili mwandamizi daraja 11 wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa(Nida)wilayani Mbinga Ibrahim Patrick alisema kwamba,vitambulisho 131,181 vitakavyogawiwa vitafikisha idadi ya wananchi 164,275 sawa na asilimia 88.3 ya wananchi waliojiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa.

Aidha alisema,vitambulisho 7,893 vimeshazalishwa na muda wowote kuanzia sasa vitapokelewa na ofisi ya Nida wilaya ya Mbinga na vitaendelea kusambazwa kwenye ofisi za watendaji kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi.

Alisema,ugawaji huo utawezesha kukata kiu ya muda mrefu ya wananchi wa Mbinga ambao wamekuwa wakisubiri kupata vitambulisho kwa muda mrefu na kuongeza kuwa, zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo litadumu kwa muda wa siku 14.


Alisema,baada ya hapo vitambulisho vilivyobaki vitarudishwa kwenye ofisi ya Nida wilaya na wananchi watakoshindwa kuchukua vitambulisho vyao ndani ya muda huo watalazimika kuvifuata kwenye ofisi ya Nida na kusisitiza kuwa,vitambulisho hivyo vinatolewa bure.

Patrick,amemuomba Mkuu wa wilaya ya hiyo Aziza Mangosongo ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,kusimamia na kuhamasisha wananchi kufika kwenda ofisi za watendaji ili kuchukua vitambulisho hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo alisema,zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa(NIDA)ni endelevu na kwamba wananchi wote waliosajiliwa watapatiwa vitambulisho na hata ambao hawajasajiriwa wanapaswa kusajiriwa ili waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Alisema,vitambulisho hivyo ni muhimu kwani vitawasaidia wananchi kutumia katika usajili wa simu na kuwezesha kupata huduma mbalimbali za kijamii na kwa ajili ya kutambulisha Uraia wao.

Mangosongo,amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu ili vitambulisho hivyo viwafikie wananchi wote na hataki kuona baadhi vinarudishwa NIDA kwa kukosa wahusika.

“vitambulisho hivi gaweni bure kwa wananchi,acheni kukaa navyo ofisini kwa muda mrefu ili kutengeneza mazingira ya kupata mshiko(rushwa) na acheni kujifanya Miungu watu wakati wa zoezi la ugawaji kwa wananchi”alisema Mangosongo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini Jonas Mbunda alisema,kwa muda mrefu kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo,hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma muhimu za kijamii.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa zaidi ya Sh.bilioni 42.5 zilizotumika kutengeneza na kusambazwa kwa vitambulisho vya Taifa kwa Watanzania wote.

Mbunga,amewataka watendaji waliopewa dhamana ya kugawa vitambulisho hivyo,kujiepusha na mambo ya ovyo ikiwemo kuomba na kupokea rushwa au kutoa vitambulisho kwa upendeleo ili kuepusha malalamiko na usumbufu kwa wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Aziza Mangosongo kushoto,akimkabidhi kitambulisho cha uraia mkazi wa mji wa Mbinga Maurus Pokela wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya uraia(NIDA)wilayani humo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...