Na Mwandishi wetu

Ili kuongeza thamani ya zao la Chai nchini Serikali imetaja mikakati inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta hiyo ikilenga katika kuimarisha minada na kuongeza thamani ya bidhaa inayozalishwa na wakulima wadogo nchini.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chai cha Sakare Specialty Tea Company (SSTC) kilichopo wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.

Kiwanda hicho kinatawajiwa kuleta mapinduzi katika kilimo na uchakataji wa chai nchini hali itakayoleta mafanikio katika mbinu za kilimo na viwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo Bashe amesema ili kuboresha sekta ya kilimo na zao la chai, mikakati mikubwa ni kuhakikisha kunakuwa na minada ya chai nchini na kubainisha kuwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo wanatakiwa kuuza bidhaa wanayozalisha katika soko la chai la Dar es Salaam.

“Hata kama kampuni itakuwa imesajiliwa katika soko la hisa la London (London Stock Exchange) chai itakayozalishwa nchi inapaswa kupita katika soko la Dar es Salaam. Wasipofanya hivyo, watafunga kiwanda chao na tutakibadilisha kuwa kiwanda cha kuuzia chuma chakavu,” amesema Bashe

Amesema kwa wastani, chai inayouzwa katika soko la Mombasa imekuwa ikitoa wastani wa Senti 0.7 ya Dola ya Marekani, kiasi ambacho kilipatikana kwenye mnada wa kwanza uliofanyika katika soko la Dar es Salaam na kuongezeka hadi Senti 0.9 katika mnada wa pili uliohusisha mauzo ya chai gredi ya chini kabisa inayozalishwa nchini.

Amesema Bashe, licha ya kufanikiwa kuongeza bei elekezi ya chai hadi Sh366 kwa kilo, wizara yake haijaridhika, hivyo aliahidi kufanyia kazi changamoto zote zinazoathiri bei ya chai nchini.

“Tutashirikiana na wizara ya Fedha kuanzisha vivutio vya kikodi katika zao la chai. Tanzania inatumia wastani wa tani milioni sita za chai kwa mwaka, lakini kampuni za ndani zimekuwa zikinunua tani milioni mbili pekee hali inayoonesha kuwa kuna kiasi kikubwa cha chai kutoka nje ya nchi katika soko la Tanzania,”

Bashe ameahidi kushirikiana na Wizara ya Fedha kuondoa chai kwenye orodha ya bidhaa zinazoingia moja kwa moja kwenye masoko ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ili kulinda zao hilo kama sukari inavyolindwa.

Katika uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kuanzisha mazungumzo na wananchi wanaoishi kuzunguka kiwanda hicho ili walipwe fidia na kuhama kupisha upanuzi wa kiwanda hicho.


Alisema wakiwa na hekta 715, wakulima watakuwa na uwezo wa kuzalisha chai ya kiorthodoksi kwa ajili ya matumizi ya ndani na mauzo nje ya nchi ambapo chai ya kawaida itazalishwa kwa ajili ya mauzo katika Soko la Dar es Salaam.

“Serikali imepata fedha kupitia mradi wa Program-for-Results (P4R) na kwamba kuna kiasi kimetengwa kwa ajili ya kuanzisha viwanda vitano vya kuongeza thamani ya chai inayozalishwa na wakulima wadogo,” alisema.
“Wataalamu wameelekezwa kuleta teknolojia itakayofungwa kwenye viwanda hivyo toka nchini India ambapo zitakuwa zimefungwa kufikia Juni 2024,” amesema

Mwenyekiti wa Bodi ya Chai (TBT) Mustafa Umande amesema zao hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kuporomoka kwa bei na kupaa kwa gharama za uzalishaji.


“Tunafanya jitihada kubwa kuongeza matumizi ya ndani chai ndani ya nchi,” alisema, akiishukuru serikali kwa kuwapatia wakulima miche ya kisasa ya chai na mbolea pasipo malipo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kazi Yetu Linus Ndongwe amesema uzinduzi huo umewaongezea ari ya kuongeza thamani, kuzalisha ajira na ubora wa chai hivyo kuifanya chai ya Tanzania itoe ushindani mkubwa katika soko la kimataifa.
 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chai cha Sakare Specialty Tea Company (SSTC) kilichopo wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga. Serikali imetaja mikakati yake katika kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya zao la Chai ikilenga katika kuimarisha minada na kuongeza thamani ya bidhaa inayozalishwa na wakulima wadogo nchini.
 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akionja Chai wakati Uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chai cha Sakare Specialty Tea Company (SSTC) kilichopo wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga huku Serikali ikitaja mikakati yake itakayoleta mapinduzi makubwa kwenye sekta hiyo ikilenga katika kuimarisha minada na kuongeza thamani ya bidhaa inayozalishwa na wakulima wadogo nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...