Na Khadija Khamis -Maelezo 18/12/2023.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulidi Mwita amesema Wizara imejipanga kuhakikisha Sekta ya habari inaimarika kwa kufanya mageuzi ya kisera na kisheria.

Hayo yamesemwa katika Ukumbi wa ZBC Karume House wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mikakati, malengo na mafanikio ya Wizara hiyo Kuelekea madhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema katika kufikia malengo ya Wizara hiyo ni vyema kubadilisha sera na sheria zilizopitwa na wakati kwa kufanya mageuzi ili kuziendeleza sekta za habari Nchini.

Aidha alieleza katika kuiendeza Idara ya Habari Maelezo wizara imerekebisha sera na sheria iliyopo na kuandaa sera mpya ya habari ya mwaka 2023 pamoja na kusimamia vitengo vya Habari na Mawasiliano vya Taasisi za Serikali kwa lengo la kuhakikisha taarifa mbali mbali za Serikali zinaifikia jamii kwa wakati.

Hata hivyo ameeleza Tume ya Utangazaji imepatiwa vifaa vya kisasa na wataalamu ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia za kisasa.

Pia Waziri Tabia amesema Katika kuimarisha shirika la Magazeti la Zanzibar shirika hilo limeweza kuengeza nakala za magazeti na usambazaji kwa Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Alifahamisha kuwa Kampuni ya Kusambaza Maudhui (ZMUX) imeandaa mpango wa kuengeza biashara na kusogeza huduma kutoka Zanzibar hadi Tanzania Bara.

Akizungumzia sekta ya vijana amesema ili kuimarisha Maendeleo ya Vijana, Wizara imetumia jumla ya Shilngi 995,152,420/= kwa ajili ya ujenzi wa Vituo 2 vya Mafunzo ya Vijana (Youth Training Centre) ambavyo vitawajengea uwezo Vijana katika maeneo mbali mbali.

Mhe.Tabia amesema wizara imefanya Makongamano matatu ya Kimataifa yakiwemo mawili ya Kiswahili na moja la Idhaa ya Kiswahili Duniani pamoja na kushiriki katika makongamano saba yaliyofanyika ndani na nje ya Zanzibar kwa lengo la kuendeleza, kukuza na kueneza Kiswahili.

Amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kusimamia na kuimarisha michezo ya Wilaya, Mikoa na Taifa kwa Kujenga na kuvifanyia Ukarabati viwanja vya Amaan stadium na Gombani Pemba Sambamba na kusajili jumla ya michezo 44, kati ya hiyo 40 ni ya kisasa na 4 ni michezo ya asili ikiwemo Nage, Karata, Bao na kulenga shabaha.

Hafla hiyo ikiwa ni muendelezo wa mahojiano baina ya Mawaziri wa Wizara mbali mbali na Waandishi wa Habari katika kuelezea maendeleo, malengo na mafanikio ya Wizara, kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na mafanikio ya Wizara hiyo kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar,hafla iliyofanyika Karume house Mjini Unguja .


Mwandishi wa habari kutoka Bomba Fm Maryam Kheir akiuliza swali kwa Waziri wa habari,vijana, utamaduni na michezo Mhe Tabia Maulid Mwita wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na mafanikio ya Wizara hiyo kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar,hafla iliyofanyika Karume house Mjini Unguja .

Mwandishi wa habari kutoka shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar leo Ameir Khalid akiuliza swali kwa Waziri wa habari,vijana, utamaduni na michezo Mhe Tabia Maulid Mwita (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na mafanikio ya Wizara hiyo kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar,hafla iliyofanyika Karume house Mjini Unguja .PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...