Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa
wito kwa viongozi mbalimbali serikalini kuhakikisha kuwa, kazi
walizonazo wanazifanya kwa bidii kubwa na kuacha alama nzuri kwa
wananchi, hivyo ni muhimu kazi hizo zikaonekana na kufaidisha
wananchi.

Amesema hayo tarehe 5 Desemba 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada
Maalum ya kuaga Mwili wa Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Erasto Kweka
iliyofanyika katika Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

Ibada hiyo Maalum ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa na Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

“Nikitolea mfano wa Marehemu Baba Askofu Kweka ameacha alama nzuri
duniani kwani ameanzisha vitu vingi ambapo hata kama ameondoka, vitu
hivyo vinaendelea kuonekana na kufaidisha wengine mfano wa enzi ya
uhai wa Baba Askofu alitoa mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya
kijamii ikiwemo kuleta usawa wa kijinsia, uanzishwaji wa miradi ya
maji safi ndani na nje ya Dayosisi, Elimu, uanzishwaji wa Chama cha
Akiba na Mikopo pamoja na Benki ya Uchumi ya KKKT ambayo inawahudumia
watu wote na madhehebu yote.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii
na kutokuta tamaa, akitolea mfano wa maisha ya Marehemu Baba Askofu
Kweka ambaye alianza kutafuta maisha akiwa kijana mdogo baada ya
kufiwa na Baba yake akiwa na umri wa miaka 14 mpaka hatua aliyofikia
sasa ya mafanikio kwa Kanisa la KKKT na watu wanapata huduma kupitia
juhudi zake.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan anatambua
mchango wa Marehemu Baba Askofu Kweka kwenye maendeleo ya Kanisa la
KKKT na kwamba Serikali itauenzi mchango wake katika Sekta pia za
Afya, Elimu na Maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania
(KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini , Dkt. Fredrick Onaeli Shoo
amesema kuwa, viongozi wa Kanisa hilo wamefarijika na uwepo wa
viongozi wa Serikali waliojumuika nao kutoka siku msiba ulipotokea
mpaka wakati wa Misa hiyo Maalum.

Pia ametoa pole kwa Wananchi na Serikali kufutia maafa yaliyotokea
katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara ambapo baadhi ya wananchi
wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa kufuatia maporomoko ya ardhi
na ameeleza kuwa Kanisa linafarijika na juhudi mbalimbali
zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika
kutatua changamoto katika eneo hilo, na tayari Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa Majaliwa yupo katika eneo la maafa na timu kutoka kwenye
ofisi yake.

Marehemu Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Erasto N. Kweka alizaliwa tarehe
24 Aprili, 1934 katika Kijiji cha Mamba Uswaa wilaya ya Hai mkoa wa
Kilimanjaro ambapo enzi ya uhai wake alitumika katika nyanja
mbalimbali ikiwemo Ualimu, kabla ya kuingia ngazi ya Utumishi wa
Kanisa.

Mwaka 1973 alichaguliwa kuwa Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya
Kaskazini wadhifa alioutumikia hadi mwaka 1976, ambapo mwaka mmoja
baadaye alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini na pia
kukaimu nafasi ya Mkuu wa Kanisa kabla ya kustaafu kwa heshima mwaka
2004.

Marehemu Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Kweka alifariki Jumamosi tarehe 25
Novemba, 2025 saa 4 Asubuhi akiwa na umri wa miaka 89.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitoa
salamu za pole kwa familia ya Marehemu Baba Askofu Mstaafu, Dkt.
Erasto Kweka, kabla ya Ibada Maalum ya Kuaga Mwili wa Baba Askofu leo
Disemba 5, 2023 Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza
na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu
wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onaeli Shoo kabla ya Ibada ya
Maalum ya Kuaga Mwili wa Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Erasto Kweka katika
Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro leo Desemba 5, 2023.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Akiaga
Mwili wa Marehemu Baba Askofu Mstaafu Dkt. Erasto Kweka, wakati wa
Ibada

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...