SERIKALI Ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA,) wameendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya Elimu ambapo kupitia Program ya JICA Chair (Program for Japanese Studies) wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,) watapata fursa ya kupata mafunzo ya Ubunifu na Ujasiriamali yatakayowasaidia wanafunzi hao kubidhaisha bidhaa za bunifu zao.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana mafunzo hayo Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi amesema; JICA imekuwa ikisaidia Serikali na wananchi katika nyanja mbalimbali na kuanzia mwaka jana wamekuwa wakishirikiana na UDSM katika nyanja ya ubunifu na katika kuendeleza hilo kuanzia Desemba 4 hadi 8 mwaka huu kutakuwa na mafunzo hayo maalum ya ubunifu yatakayoendeshwa na wakufunzi kutoka Japan kwa njia ya mtandao ili kuwapatia ujuzi wanafunzi hao ambao baadaye watashiriki mafunzo kwa vitendo katika viwanda mbalimbali.

Hitoshi amesema, ili kufikia malengo katika biashara vitendo na ubunifu vinahitajika na kusisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa sekta binafsi katika Nchi zinazoendelea hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa vijana katika kuongeza idadi ya sekta binafsi hali itakayochagiza ukuaji wa uchumi kwa Taifa, kuongezeka kwa ajira na kukuza jamii kwa ujumla.

Amesema, sekta binafsi zina mchango mkubwa katika kuyafikia mafanikio na kupitia kongamano litakalofanyika Desemba 5, vyuo vikuu na sekta binafsi kutoka Japan zikiwemo TOYOTA na HONDA pamoja na chuo kikuu cha Tokyo wataeleza uzoefu katika bunifu kwa kuhusianisha na ukuaji wa uchumi.

Pia, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof. Hannibal Bwire amesema JICA kupitia program hiyo wamekuja kusaidia jitihada za kuwapatia vijana maarifa juu ya masuala ya ubunifu na ujasiriamali ili wakihitimu waweze kujiajiri na kuajiriwa.

"Kupitia kongamano la ujasiriamali lililofanyika Februari mwaka huu na watu zaidi ya 600 wakishiriki, Japan walieleza namna walivyomove kutoka katika vita kuu ya dunia hadi kufikia Dunia ya kwanza ya maendeleo kama inavyofahamika.....wamekuja kusaidia jitihada za UDSM kupitia mafunzo ambayo makundi matatu kati ya sita yatachaguliwa na yatatekeleza mawazo ya ubunifu na ujasiriamali kwa vitendo ndani ya wiki sita." Amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Ujasiriamali kutoka Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Dr. Winnie Nguni amesema, Program hiyo imelenga kusaidia wanafunzi kufikiri bunifu zao katika mlengo wa kibiashara.

"Tumegundua kuwa wanafunzi wengi wana uelewa na ujuzi sana ufundi wa kutengeneza bidhaa na wanakosa ujuzi, uelewa na maarifa ya kubiasharisha bidhaa zao...kupitia program hii tunaamini wanafunzi wengi zaidi watapata maarifa ya namna bora ya kufikia malengo yao na kufanikisha mawazo yao kibiashara." Amesema.

Dr. Winnie ameeleza, kupitia program hiyo inayofadhiliwa na JICA kwa wanafunzi wa UDSM itawapa maarifa mbalimbali kuanzia namna ya kuunda bidhaa, kubidhaisha kwa kufikiri zaidi katika masoko, namna ya kupata fedha ya kutekeleza mawazo hayo na katika kuajiri kwa kuangalia watu wa namna gani watakaowasaidia kufikia malengo yao.

Aidha amesema kuwa, program hiyo pia itawasaidia katika kuchangamana na watu wengi zaidi na kuangalia namna ya kuendesha biashara zao hali itakayopunguza changamoto kwa wanafunzi na wahitimu kushindwa kusimamia bunifu zao kwa kukosa maarifa hayo pindi watakapohitimu masomo yao.

Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Ara Hitoshi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani,) kuhusiana na mafunzo hayo na kueleza kuwa vitendo na ubunifu ni nguzo katika kuyafikia malengo ya biashara. Leo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof. Hannibal Bwire akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani,) juu ya mafunzo hayo na kueleza kuwa yatawasaidia vijana katika kuendeleza bunifu zao, kujiajiri au kuajiriwa. Leo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Ujasiriamali kutoka Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Dr. Winnie Nguni akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani,) kuhusiana na mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali yatakayowanufaisha wanafunzi wa chuo hicho kwa ufadhili wa JICA, amesema wanafunzi watanufaika na kuweza kuendeleza mawazo yao bunifu baada ya kuhitimu masomo yao. Leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...