Mwezeshaji Dkt.Ummulkulthum Omar akiwasilisha mada ya afya na matatizo ya mfumo wa uzazi katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wanawake juu ya afya ya uzazi na ujasiriamali huko Michezani mall mjini Unguja.
Mratibu wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wanawake juu ya Afya ya uzazi na ,ujasiriamali Raya Hamad Sleiman akitoa maelezo mafupi kuhusiana na mafunzo hayo huko Michezani mall mjini Unguja.
Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Abeda Rashid Abdalla amewataka wanawake kuchangamkia fursa za mikopo ili kuendeleza ujasiriamali na kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza na wajasiriamali wanawake wakati akizindua mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya afya ya uzazi na ujasiriamali amesema Serikali imekua ikitoa mikopo kwa wajasiriamali kupitia wakala wa uwezeshaji wananachi kiuchunmi ZEEA hivyo ni vyema kaikimbilia fursa hiyo ili kuepuka kuwa tegemezi na ombamba.
Alisema ujasiriamali ni kazi ngumu ambapo wanawake wengi hushindwa kufikia malengo kwa kutokuwa tayari kujituma na kujitoa jambo linalopelekea kuwa mzigo kwa familia na Serikali pamoja na kuongeza idadi ya ombaomba nchini.
Akizungumizia kuhusu udhalilishaji amesema licha ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali tatizo hilo bado ni janga la taifa hivyo ipo haja ya kushirikiana kuendelea kuhamasisha jamii juu ya kumaliza janga hilo.
Hata hivyo aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao bila kujali jinsia na kuwadadisi hali wanazokutana nazo wanapokuwa nje ya majumba yao.
“Kila mwezi idadi ya wanaotoa taarifa za udhalilishaji inaongezeka na hao ni wale wanaotoa taarifa tu hatujui wanaomalizia kesi hizi majumbani kwao”alisema bi Abeda
Akitoa maelezo mafupi mratibu wa mafunzo hayo Raya Hamad Sleiman amesema lengo kuu la mafunzo hayo kwa wajasiriamali ni kuona wanapiga hatua za kimaendeleo na kuweza kuanzisha mitaji ya kuwapeleka mbele kiuchumi, kujitambua na kuweza kupambana na udhalilishaji.
pia aliwataka wanawake hao kuwa mabalozi wazuri wa kuihamasisha jamii juu ya kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kujikinga na maradhi ya kuambukiza na yasiyo yakuambukiza.
Akiwasilisha mada ya afya na matatizo ya mfumo wa uzazi Dkt.Ummul-kulthoum Omar amesema kujikinga na maradhi ni bure na kujitibu ni gharama kubwa hivyo ipo haja ya jamii kutafuta elimu ya afya kila kona ili kuepuka gharama za kujitibu.
Amesema miongoni mwa matatzio yanayowakumba wanawake katika mfumo wa uzazi ni pamoja na maumivu makali wakati wa hedhi, kukosa hedhi ,mayoma ,PID, homoni,pamoja na maumivu wakati wa tendo la ndoa hivyo aliwanasihi wanawake hao kutokuficha maradhi hasa ya mfumo wa uzazi kwani yanapokomaa ni vigumu kutibika na kupelekea kukosa kizazi.
Alifahamisha kuwa Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imekuwa ikiajiri madaktari bingwa wa kila kada hivyo kuwataka kina mama kuacha kufuatilia maradhi na tiba mtandaoni na kufika hospitali mara tu wanapoona dalili za maradhi hayo.
Aliwashauri wanawake kuwa na utaratibu mzuri wa kujisafisha na kuacha kutia vitu ukeni kwani huuondoa walinzi wa uke na kukaribisha vimelea na bakteria wanaosababisha maradhi ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.
“kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi mara kwa mara ili kuimarisha afya zetu na kupunguza gharama za matibabu pale yanapokua makubwa,maradhi kutibiwa mapema ni bora.” Alisema Dkt. Ummy
Aidha alifahamisha kuwa Serikali inashajihisha kupatiwa chanjo ya HPV wasichana wa miaka 14 na chanjo hiyo ni salama na kuwataka kinamama kuwa na utamaduni wa kuchunguza shingo ya kizazi kila baada ya miaka 3.
Mwezeshaji Zuleikha Mohamed akiwasilisha mada ya ujasiriamali amesema ili uweze kuwa mjasiriamali mkubwa ni lazima kuangalia ushindani wa kibiashara, kuwa mbunifu pamoja na pamoja na kuitumia vyema mitandao ya kijamii katika kutangaza biashara.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Sabrina Ali khamis na Mgeni Nassir khamis walishukuru kupatiwa nafasi hiyo inayoenda kuwa chachu ya kuleta mabadiliko pamoja na kutoa wito kwa wadau na Serikali kuendeleza mafunzo kama hayo ili jamii iweze kujitambua kujiajiri na kuacha kuwa tegemezi .
MAFUNZO hayo ya siku moja yaliandaliwa na BANATY EMPOERMENT na kuwashirikisha wajasiriamali wanawake na mada mbali mbali ziliwasilishwa ikiwemo Afya na matatizo ya mfumo wa uzazi, ujasiriamali na kujitambua ikiwa ni zawadi kwa wanawake hao kutoka kwa taasisi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...