Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo amekabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC) Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kati ya washindani 500 kutoka nchi mbalimbali dunia.

Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Global Centre on Adaptation (GCA) jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambako unafanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28).

Akikabidhi tuzo hiyo kwa Kiongozi wa Baraza hilo kutoka jamii ya Kimasai Bi. Maanda Ngoitiko aliyeipokea kwa niaba ya Baraza hilo, Dkt. Jafo amewapongeza kwa kuipatia Tanzania sifa.

“PWC wameiheshimisha sana Tanzania na kuifanya isikike duniani na nina uhakika kabisa tuzo hii imetokana na juhudi binafsi za dada yangu Maanda za kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake wafugaji kwa kuwajengea uwezo kiasi cha kufikia usawa katika kutoa maamuzi katika jamii zao,” amesema Waziri Jafo.

Akishukuru kwa tuzo hiyo Bi. Maanda amesema kuwa Baraza hilo linawahudumia wanawake na wasichana kutoka jamii za Wamasai, Sonjo, Akie na Barabaig.

Ameongeza kuwa PWC ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kaskazini mwa Tanzania kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake na wasichana wa Kimasai.

Wakati huo Tanzania inaendelea kushiriki katika Mkutano wa COP 28 sanjari na mikutano ya pembezoni (side events), mikutano ya uwili (bilateral meetings) na warsha ambapo watu zaidi ya 81,000 kutoka nchi zaidi 190 wanahudhuria.

Tanzania imeandaa banda la maonesho katika viwanja vya Dubai Expo City likisheheni wizara na taasisi mbalimbali ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais inawakilishwa na Waziri Dkt. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga na wataalamu kutoka Ofisi hiyo.

Aidha, Mkutano huo unaochagizwa na kaulimbiu ya kitaifa ‘Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi‘, ulifunguliwa rasmi Novemba 30 na unatarajiwa kuhitimishwa Desemba 12, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akikabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC) Tanzania, mshindi wa kwanza kati ya washindani 500 dunia iliyotolewa na Taasisi ya Global Centre on Adaptation (GCA) kwa Kiongozi wa Baraza hilo kutoka jamii ya Kimasai Bi. Maanda Ngoitiko jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambako unafanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28).

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu mara baada ya kukabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC) kupitia kwa Kiongozi wake Bi. Maanda Ngoitiko (wa pili kushoto).

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...