Na. Mwandishi wetu Bungeni-Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendesha mafunzo ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu kwa Askari wanyamapori wa vijiji wapatao 24 kutoka Wilaya ya Manyoni. Mafunzo haya ambayo yanatarajiwa kukamilishwa Mwishoni mwa mwezi Februari 2024 yanaendeshwa katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga kilichopo mkoani Ruvuma.

Haya yamebainika leo Bungeni wakati Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) akijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki ambaye alitaka kujua Je nini mkakati wa serikali wa kudhibiti tembo wanaoathiri wakulima wa korosho wa tarafa ya Nkonko?

Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori nchini, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020-2024.

Mhe. Kitandula aliongeza kuwa katika vijiji vya Nkonko, Mpola na Mpapa vilivyopo katika Tarafa ya Nkonko, Serikali kupitia Wizara imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu za kukabiliana na wanyampori wakali na waharibifu hususan tembo ili kuwajengea wananchi uwezo.

‘Sambamba na jitihada hizo, Wizara imejenga kituo cha askari wa wanyamapori katika Kijiji cha Nkonko kilichopo Tarafa ya Nkonko. Aidha, kwa mwaka 2023/24 Wizara imepanga kujenga kituo cha Askari wa wanyamapori katika Makao Makuu ya Pori la Akiba Kizigo kwa ajili ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika Tarafa zenye changamoto hiyo ikiwemo Nkonko’ alisema Mhe. Kitandula.

Kwa upande wa ulipwaji wa kifuta jasho na kifuta machozi Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Wizara imeshatoa zaidi ya shilingi milioni 69 katika wilaya ya Manyoni kwa ajili ya kifuta jasho na kifuta machozi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2022/23, na kwamba kwa mwaka 2023/24 matukio 226 yameripotiwa na kufanyiwa tathmini; na sasa wizara ipo kwenye hatua za mwisho za kufanya uhakiki ili wananchi wanaostahili waweze kupatiwa kifuta jasho na kifuta machozi.

Kuhusu jitihada za Wizara katika kukabiliana na tatizo la Mamba, Mhe. Kitandula alilieleza bunge kuwa Taasisi ya Utafiti wa wanyamapori (TAWIRI) imebuni mfumo wa kuwalinda wananchi kwa kutumia vizimba vinavyojengwa kwenye maeneo ambayo wananchi wanayatumia kuchota maji na shughuli nyingine za kibinadamu kwenye maeneo yenye tatizo la mamba.

Aidha, ametoa rai kwa Halmashauri zinazokabiliwa na changamoto hii kutenga fedha kwenye bajeti zao zitakazowezesha kugharamia uwekaji wa vizimba kwenye maeneo yao yenye changamoto ya mamba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...