MKURUGENZI wa Utafiti na Sera za Uchumi katika Benki Kuu ya Tanzania( BoT) Dkt. Suleiman Missango amesema benki hiyo imeanzisha Mfumo Mpya wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate),Amesema kuanzishwa kwa mfumo huo mpya kunafuta mfumo uliokuwepo wa ujazi wa fedha uliodumu kwa miaka 28, toka mwaka 1995 na umefikia kikomo mwaka 2023.

Akizungumza leo Januari 9, 2024 jijini Dar es Salaam mbele ya Wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini, Dk.Missango amesema Januari mwaka huu BoT itatangaza kwa mara ya kwanza kiwango cha RIBA, chini ya utaratibu huo mpya.

Dkt. Missango aliyekuwa akielezea Mfumo Mpya wa Uandaaji wa Sera ya Fedha (Interest Rate-Based Monetary Policy Framework) na Ukusanyaji wa Sarafu, kwa Wahariri wa habari za biashara na uchumi amesema sababu ya mabadiliko hayo ni kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa sera ya fedha katika kusimamia malengo mapana ya kiuchumi ya kudumisha utulivu wa bei (Inflation Stability) na ukuaji wa uchumi (Economic Growth) na pia kuongeza uwazi.

“Kuhama kwenye mfumo wa ujazi kwenda kwenye riba ni sehemu ya uboreshaji wa Sera ya Fedha katika kufikia malengo ya Sera ya Fedha ambayo ni kudhibiti mfumuko wa bei na kusaidia ukuaji wa uchumi kulingana na mipango ya serikali.

"Utekelezaji wa Mfumo wa Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate) umeonesha matokeo mazuri katika usimamizi wa sera ya fedha na kuimarisha misingi ya utekelezaji wake katika mazingira ya uwazi katika nchi mbalimbali duniani na kutoa mfano wa Ghana, Afrika Kusini, Mauritius na kwa Afrika Mashariki nchi ya kwanza kutumia mfumo huu, ametaja kuwa ni Uganda."

Aidha kidunia nchi ya kwanza ilikuwa New Zealand, iliyofuatiwa na Uingereza mwaka 1990, amesema Mchumi huyo mbobezi nchini.

Pia amesema sababu nyingine ni kwamba mfumo huo wa kutumia riba kwa mazingira ya Tanzania utaondoa usimamizi wa ujazi (Quantity) na badala yake utaangalia bei (Price) huku akifafanua mfumo huo mpya utazisaidia Benki kuimarika zaidi na kupanga riba.

Amesisitiza kuwa lengo la BoT ni kudhibiti mfumuko wa bei ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa nchi, riba itakuwa ni kiashiria cha mwenendo wa uchumi wa nchi.

Kuhusu malengo ya Sera ya Fedha, Dkt. Missango amesema ni pamoja na kuhakikisha kiwango cha fedha kilichopo kwenye uchumi kinakidhi mahitaji ya Shughuli za Uchumi

“Kiwango kikubwa cha fedha katika mzunguko zaidi ya mahitaji ya shughuli za uchumi hupelekea kuongezeka kwa bei za huduma na bidhaa (mfumuko wa bei) wakati kiwango kidogo kisichokidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi hupelekea kuzorotesha shughuli za uchumi.

"Na kudumaza ukuaji wa uchumi, na hivyo, utekelezaji wa sera ya fedha unalenga kuweka utulivu wa bei za bidhaa na huduma na kuwezesha shughuli za uchumi kufanyika ipasavyo," amesema Dk.Missango.
Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango, akizungumza na Wahariri wa habari za biashara na uchumi, kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, leo Januari 9, 2024.
Meneja Uhusiano BoT, Bi. Vicky Msina akifafanua jambo mbele ya Wahariri wa habari za biashara na uchumi (hawapo pichani), kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, leo Januari 9, 2024.wakati semina hiyo ikiendelea.


Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango, akizungumza na Wahariri wa habari za biashara na uchumi, kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, leo Januari 9, 2024.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...