-Akabidhi Pikipiki na kofia ngumu Jumuiya ya Wazazi (CCM) Zanzibar

-Awataka kutumia pikipiki hizo kuieneza CCM

-Azuru Kaburi la Hayati Abeid Amani Karume

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka
Jumuiya ya Wazazi ya CCM kutumia rasilimali walizonazo katika
kukijenga na kukieneza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo
mbalimbali ya nchi na kuzungumza na wananchi kuhusu kazi kubwa za
maendeleo zinazofanywa chini ya Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Doto Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
(Kundi la Wazazi), amesema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa
Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk. Kikao kilifanyika katika Afisi
Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi.

“Kama wewe ni Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wa Mkoa au kiongozi yoyote
yule, kwa kutumia rasilimali ulizonazo tembelea maeneo ya mkoa wako,
Wilaya na Vijiji hata mara moja, zungumza na makundi mbalimbali
ikiwemo Wajumbe wa Kamati za utekelezaji za Jumuiya yetu na waeleze
kuhusu masuala ya kujenga na kueneza Chama. Hii inawezekana,
tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya
makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio
ambayo CCM na Serikali yake wameyafanya.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni Jumuiya kubwa
ndani ya Chama hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga Chama kwa
ukubwa huo kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka
au ukomo wa mtu kuwa sehemu ya Jumuiya.

“ Nikitolea mfano Jumuiya yetu ya Wanawake, inahusu Wanawake katika
Chama, Jumuiya ya Vijana umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo,
lakini Jumuiya hii haina mipaka hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa,
tutumie ukubwa wa Jumuiya hii kuwasaidia Mwenyekiti wetu na Makamu
Mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga Chama na kuzungumza kwa
ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika.” Ameeleza Dkt.
Biteko

Ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu
Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi wanataka
kuona viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi
ikiwemo ya kueleza mafanikio makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea
kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika
kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa
nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa,
Dogo Mabrouk amemshukuru Dkt.Biteko kwa kuithamini Jumuiya hiyo na kwa
kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji wa Jumuiya
kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa
ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Dkt. Biteko alizuru katika Kaburi
la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo
Kisiwandui Zanzibar.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekabidhi PikiPiki Sita kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi (CCM),
Zanzibar pamoja kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya hiyo kwenye Mikoa
Sita ya Zanzibar.

Amesema kuwa, pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) ambapo
ameelekeza kuwa, pikipiki hizo zikafanye kazi ya siasa kama
ilivyokusudiwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiomba dua katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk. Kikao kilifanyika katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa
Mjini Magharibi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambayeni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), akikabidhi pikipiki Sita na kofia ngumu kwa Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar. Makabidhiano yalifanyika katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...