NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA.

MLINZI wa makaburi ya Waislamu jijini Mwanza,Shakrani Ramadhan Haruna,anadaiwa kufanyiwa ukatili na Kamati ya Mpito ya Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza,baada ya kukataa kumlipa mshahara kwa zaidi ya miaka sita,kwa madai haina mkataba naye.

Hali hiyo imesababisha mlinzi huyo kugeuka omba omba baada ya waajiri wake hao kutomlipa ujira wake yakiwemo mapunjo na mambikizo ya mshahara sh. 22,775,000 tangu watwae madaraka ya kusimamia msikiti huo baada ya bodi iliyokuwepo kuvunjwa.

Akizungumza kwa uchungu leo, Shakrani amesema tangu Kamati ya Mpito ya Msikiti wa Ijumaa itwae madaraka Julai 2018 hadi sasa 2024,ikiongozwa na Sheikh Aman Mauba,imegoma kumlipa ujira wake ikidai haina mkataba naye na kusababisha kuishi maisha ya shida na familia yake ya watu 12.

“Nimefanya kazi ya ulinzi wa makaburi ya waislamu yaliyopo Mlango Mmoja kwa miaka 16 nikilipwa mshahara wa sh. 150,000 kwa mwezi,matatizo ya kutolipwa yalianza Julai 2018 baada ya Kamati ya Mpito chini Mwenyekiti,Sheikhe Amani Mauba kuingia madarakani,”amesema.

Shakrani amesema kutolipwa fedha hizo sh. 22,775,000 za mapunjo na malimbikizo ya mishahara alimfuata aliyekuwa Katibu wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa iliyovunjwa,Sheikh Abdallah Amin Abdallah akamweleza kufunga kwa akaunti ya msikiti na RITA,hivyo mshahara wake atalipwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito (Sheikh Mauba) kwa niaba ya bodi.

“Niliufuata tena uongozi wa kamati hiyo kudai mshahara wangu lakini Sheikhe Mauba akasema aliyeniajiri hakunikabidhi kwao ambapo Septemba 7,2023 niliitwa na Imamu wa Msikiti huo,Sheikh Hamza Mansour akaniambia hawanihitaji niendelee na kazi,wataniita wanipe haki yangu lakini hawakutekeleza,”amesema Shakrani.

Pia,amewahi kufikisha madai yake ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana (DC) ambapo Katibu Tawala (DAS) akawaita viongozi wa Kamati ya Mpito bila yeye (Shakrani) kuwepo baadaye alijibiwa kwa mdomo na DAS kuwa viongozzi hao wamemkana.

“Walikukana kuwa wao si waajiri wako bali wanakuona ukifanya kazi ya ulinzi wa makaburi.Waliomba ofisi ya DC kwa heshima ya dini wahamishe shauri lako ili wakulipe na wakakubaliwa,”amesema Shakrani akinukuu majibu ya DAS.

Amesema kuwa hakuishia hapo bali alikwenda Mahakama ya Kadhi ambapo kamati hiyo iliweka mawakili wao wakidai hawamtambui na kwamba makaburi hayo anayolinda si mali ya Msikiti wa Ijumaa bali ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

Aidha BAKWATA Mkoa wa Mwanza iliwaita viongozi wa Kamati ya Mpito Sheikhe Amani Mauba (Mwenyekiti), Idrisa Haeshi (Katibu) na Imamu wa Msikiti wa Ijumaa,Sheikh Hamza Mansour (Mjumbe),wakakiri kudaiwa sh. 22,775,000 na wakaahidi kwa maandishi kulipa kiasi cha fedha kama shukurani ndani ya siku 10 za Novemba 2023 lakini hawakutekeleza.

“Fedha hizo sh.22,775,000 ni mapunjo na malimbikizo ya mshahara niliyofanya kazi miaka 16.Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Sheikh Hasani Kabeke aliniita akiwepo wakili akafanya hesabu kiwango kikashuka na kubaki sh.milioni 16 nikaridhia lakini tangu muda huo sijapata stahiki zangu,”amesema na kuiomba serikali imsaidie kupata haki yake.

Kauli ya Kamati Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito Sheikhe Amani Mauba alipoulizwa kuhusu madai hayo alikiri kuyatambua na kuomba apewe muda akutane na wenzake ili kuwa na majibu ya maamuzi ya pamoja.

“Suala hili nakiri kulifahamu lakini lina utata,wakati tukitwaa madaraka bila kukabidhiwa na bodi/serikali,hatukukuta nyaraka ya kuonyesha alikuwa akilipwa sh.100,000 au 150,000.Shida na dhamira ni namna ya kukaa tumlipe sh.ngapi,nipe muda hadi Jumatatu niwarudie wenzangu tukae kamati tuwe na maamuzi ya pamoja na si ya pekee yangu,”alisema Mauba kwa simu.

Mwandishi wa habari hizi aliwasiliana kwa simu na Sheikh Mauba ambapo alijibu kuwa; “Sina majibu na hatujakaa kujadili jambo hilo,hivyo tunashindwa tumlimpeje.Naomba unitafute baada ya siku tatu.”

Hata alipotafutwa baada ya siku hizo alizoahidi kupita amesema;“Hatujakaa bado,niko na polisi huku makaburini ukuta umebomolewa,lakini leo saa 11:00 jioni tutajitahidi tupate majibu ya Shakrani maana siwezi kutoa maamuzi ya pekee yangu na kamati ya mpito si Mauba pekee yake pia mlalamikaji tumemwuliza hana mkataba wa ajira.”

Hata hivyo,alipobanwa zaidi Sheikhe Mauba ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Wilaya ya Nyamagana,alikata simu na hata alipopigiwa iliita bila kupokewa kisha ikazimwa kabisa.Kabidhi Wasii Mkuu (RITA),Frank Kanyusi akizungumza kwa simu leo kuhusu madai ya mshahara wa Shakrani amesema hana taarifa hiyo na kumtaka aindikie kamati ya mpito barua ya madai yake ili atakapokuja Mwanza ashughulikie.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...