WAKATI Tanzania na dunia kwa ujumla ikipambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana, matumizi ya nishati jadidifu yanatajwa kuwa suluhu ya changamoto hizo.

Nishati jadidifu imetajwa kuwa chanzo cha kupunguza matatizo hayo kwa kuzalisha umeme wa uhakika na kutoa nafasi ya ajira kupitia nishati hiyo.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya CSI Energy Group, Natacha Emilien akishukuru baada ya uteuzi huo na akitaja dira ya kampuni hiyo inayojihusisha na nishati.

“Nishati mbadala hunufaisha matabaka yote ya jamii kwa usawa zaidi, hasa wajasiriamali wadogo kutokana na upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu, kutoa mafunzo.

“Pia inasaidia katika kushirikiana na wajasiriamali wanawake kama wakandarasi wadogo katika mnyororo wa thamani,”amesema Natacha.

Akizungumza katika kongamano la mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika jijini hapa Novemba 2022, Mkurugenzi wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, Dk Sixbert Mwanga alisema tafiti nyingi zinaonyesha Tanzania ina kiwango kikubwa cha nishati safi inayotosheleza mahitaji ya wananchi wake.

Alisema nishati jadidifu ni chanzo kingine muhimu kitakachowezesha uzalishaji umeme bora kwa bei rahisi na kutosheleza mahitaji ya nchi.

“Nishati mbadala zilizopo ukifuatilia zinatosha na uzuri wa hizi hazihitaji kufuatwa na gridi ya Taifa, badala yake zenyewe ndiyo zinaifuata gridi ili ziende kufidia wengine wenye upungufu.”


Jitihada za Tanzania katika nishati jadidifu


Wakati bosi wa CSI akitaja faida za matumizi ya nishati jadidifu kwa wananchi, Tanzania miezi michache iliyopita imetoka kusaini mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Irena) ambao utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji wa nishati isiyo rafiki.

Oktoba 31, 2023 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alitaja faida za mkataba wa Irene alipokuwa akiwasilisha azimio la mkataba huo bungeni jijini Dodoma.

Dk.Biteko alisema mkataba huo utasaidia kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii,  pia kutatua changamoto ya vyanzo vya umeme visivyo endelevu na uhakika.

Faida nyingine ni nchi kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu masuala ya nishati jadidifu, fursa za uwekezaji katika nishati hiyo zilizopo, kuimarika kwa utaalamu, teknolojia, utafiti na uelewa kuhusu nishati jadidifu kwa watoa maamuzi na wadau mbalimbali wa nishati

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...