Na. Khadija Ibrahim, WF, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameliambia Bunge, Mjini Dodoma kuwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi Desemba 2023, imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani zaidi ya shilingi trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya shilingi trilioni 3.1 yaliyowasilishwa.


Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa ama kukataa kuwalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki.


“Jumla ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyowasilishwa kwa uhakiki yalikuwa zaidi ya sh. bilioni 3,110.33, kati ya kiasi hicho madeni yaliyolipwa ni zaidi ya sh. bilioni 2,128.54 ambapo sh. bilioni 1,032.13 ni madeni ya wazabuni na sh. bilioni 1,096.41 ni madeni ya wakandarasi” alisema Dkt. Nchemba


Alisema kuwa madeni ya sh. bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari, pamoja na makosa ya ukokotoaji.


Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo na uchumi wa Taifa, imeendelea kutenga na kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyohakikiwa na kukubaliwa.


Alifafanua kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa madai ya wazabuni na wakandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi (certificates).

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, kuhusu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki, bungeni Jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (kulia), bungeni Jijini Dodoma.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WF, Dodoma)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...