Wazazi wameaswa kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu zaidi na kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na maskioni ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo.

Kauli hiyo imetolewa na Jopo la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo, Mapafu na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wameshiriki kuondoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Daktari Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji, Dkt. Mwanaada Kilima amesema, shanga hiyo iliingia kwenye pafu baada ya kumpalia mtoto alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.

Dkt. Kilima amesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila madhara yoyote.

“Tulitumia mpira laini wenye kamera ya video ya mapafu (Flexible bronchoscope) na kifaa cha kukamatia (foreign body basket) na kufanikiwa kuitoa hivyo kumwepusha na upasuaji mkubwa ambao ungesababisha ama kutoa pafu au sehemu ya pafu” amesema Dkt. Kilima.

Dkt. Ramadhan Hamis, Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo ndiye aliyeoongoza jopo hilo kwa kushirikiana na Dkt. Charles Komba Bingwa wa Upasuaji Kifua pamoja na Dkt. Mwanaada Kilima Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...