Mradi wa Kongani ya kisasa ya viwanda Modern Industrial Park ,Disunyara ,Mlandizi Kibaha, Mkoani Pwani (KAMAKA) inayojenga viwanda 202 katika eneo la ukubwa wa ekari 1077 imefikia asilimia 93 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ambao utakamilika mwezi Februari mwaka 2024.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji(Mb.) Januari 09,2024 alipotembelea eneo la Mradi huo katika eneo la Disunyara/Kikongo, Mlandizi wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kujionea utekelezaji unavyoendelea na kuona changamoto zilizopo ili kuzibeba na kwenda kuzifanyia kazi kupitia Mawaziri wa kisekta.

Alisema Tanzania iliamua isiachwe nyuma na mapinduzi ya nne na kuelekeza nguvu katika maendeleo ya viwanda ili kujenga nchi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoishia mwaka 2025 ambayo imeelekeza kuwe na viwanda

“Tumeunganisha jitihada kuhakikisha malengo yanatimia na tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake ulioonesha kuwa ujenzi wa uchumi nchi upo mikononi mwa sekta binafsi,” alisema Dkt. Kijaji na kuongeza kuwa mwekezaji wa Mradi huo ni KAMAKA COMPANY LIMITED wa Dar es Salaam akishirikiana na Serikali ya Tanzania.

Alisema kupitia uwekezaji huo malengo ya vijana milioni moja wanaohitimu katika vyuo mbalimbali wanaweza kufikiwa kwa ajira na Serikali iko tayari kushirikiana ili malengo ya uwekezaji huo yaweze kufanikiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza kuwa barabara ya kuanzia Makofia -Mlandizi -Mzenga -Vikumburu -Mloka ni muhimu kwani inapitia eneo la uwekezaji na miradi ya kimkakati na kuomba ujenzi huo ukianza uanzie Mlandizi kwa maslahi mapana ya eneo hilo.

Akisoma taarifa ya Mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Afriq Engineering and Construction Company Limited Mhandisi Charles Bilinga alisema makadirio ya awali yanaonesha kuwa ajira zisizopungua 200,000 zitatokana na mradi huo ulioanza Oktoba 2021 kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kongani ambapo ajira za moja kwa moja zinakadiriwa kuwa 30,000 na pato la Serikali litaongezeka kupitia Kodi mbalimbali

Mhandisi Bilinga alisema gharama za mradi huo hadi kukamilika ni sh trilioni 3 na bilioni 500 na kati ya fedha hizo sh bilioni 122 na milioni 400 zitatumika kujenga miundombinu yote ndani ya kipindi cha miaka mitano nahadi sasa kiasi cha sh bilioni 35 zimetukima kwa ujenzi w amiundombinu.

Kwa upande wake Ofisa Fedha na Masoko wa Turnkey Real Estate wauzaji wa viwanja kwenye mradi huo Bw. Tumaini Kabengula alisema mpaka sasa kuna mikataba 10 ya ununuzi wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda,kuna viwanja 24 vilivyoshikiliwa vikisubiri kusainiwa kwa mkataba, wawekezaji watatu wamekwishaanza hatua za awali za ujenzi na wengine watano waliosaini mikataba wataanza mwaka huu.

Alisema wawekezaji waliotembelea kongani kwa nia ya kuwekeza ni 58 wakitokea India China, Urutuki, Sudan ya Kusini, Afrika Kusini, Rwanda, Somalia, Tanzania, Pakistan, Yemeni, Zambia, Falme za Kiarabu, Misri, Uganda, Kenya na Canada.

Mradi huo ulianza kutekelezwa oktoba 2021 ,kwa awamu ya kwanza kwenye ujenzi wa lango kuu na uzio, kituo cha polisi, jengo la utawala, ofisi na jengo la makazi ya wafanyakazi wa zimamoto, zahanati, kituo cha umeme wa megawati 54 , mfumo wa barabara za nje na ndani na umefikia asilimia 93" alibainisha Mhandisi Charles Bilinga.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji akimsikiliza Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Ujenzi ya Afriq, Mhandisi Charles Bilingi (kulia) aliyekuwa akitoa maelezo hukusu mradi  wa Kongani ya kisasa ya viwanda iliyopo katika eneo la Disunyara na Kikongo Mlandizi Kibaha pwani jana  wakati wa ziara yake kutembelea eneo la mradi huo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge





Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa ziara yake kutembelea eneo la mradi wa Kongani ya kisasa ya viwanda iliyopo katika eneo la Disunyara na Kikongo Mlandizi Kibaha pwani jana. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Ujenzi ya Afriq, Mhandisi Charles Bilingi (wa pili kulia)  na maofisa wengine






 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...