Na Mwandishi Maalum,
Songea

WANANCHI wa kijiji cha Muhukulu na Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali kupitia wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura)kuwajengea daraja la kudumu katika mto Njoka linalounganisha vijiji hivyo na makao makuu ya wilaya Songea mjini na nchi jirani ya Msumbuji.

Walisema,daraja hilo limewasaidia sana kusukuma maendeleo yao na kumaliza usumbufu wa muda kwa kuvuka kwenye maji kila wanapotaka kusafiri kwenda maeneo mengine ikiwemo makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

Yustin Miti mkazi wa Muhukulu alisema,awali walipotaka kwenda Songea na kijiji jirani cha Kizuka na Magagula walilazimika kuzunguka hadi wilaya jirani ya Mbinga ambako ni umbali mrefu,hivyo kuwapotezea muda mwingi ambao wangeweza kutumia katika shughuli za maendeleo.

Miti alisema,hali hiyo ilichangia sana kuongeza kwa gharama za maisha kwani walilazimika kutumia kati ya Sh.15,000 hadi 25,000 kama nauli ya kutoka Muhukulu hadi Songea mjini kila wanapotaka kwenda kwa shughuli zao.

Alisema,katika mto huo kulikuwa na daraja la miti ambalo lilileta madhara makubwa kwa watu hasa wakati wa masika kwa kusombwa na maji na wengine wamepoteza maisha yao.

Paulina Mzungu alisema,baada ya kukamilika kwa daraja hilo sasa shughuli za usafiri na usafishaji wa mazao zinakwenda vizuri tofauti na zamani na amewapongeza Tarura kwa ujenzi wa mradi huo wa daraja.

Hata hivyo,ameiomba serikali kuendelea kuboresha barabara inayounganisha kijiji cha Muhukulu- Kizuka hadi Matomondo kwa kujengwa kwa lami ili iweze kupitika majira yote ya mwaka kutokana na kuharibika kila inapofika wakati huu wa masika.

Eva Komba mkazi wa Kizuka alisema,baadhi ya vijana walitumia changamoto ya kukosekana kwa daraja katika mto huo kama fursa kwani walikuwa wanavusha watu kwa fedha ambapo kwa usafiri wa baiskeli gharama yake ilikuwa Sh.500 na pikipiki 1,000.

“sasa tunapita kwa urahisi,hakuna gharama yoyote na daraja hili serikali imetutendea sana haki sisi wananchi wa maeneo haya ambao wengi wetu ni wakulima”tunamshukuru sana Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan”alisema.

Kwa upande wake kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Davis Mbawala alisema,ujenzi wa daraja hilo ulianza mwezi Disemba 2022 na kukamilika mwezi Oktoba 2023 na limejengwa kwa gharama ya Sh.696,892,665.

Alisema,daraja hilo limekamilika na linatumika kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa hasa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni na amewataka wananchi kuhakikisha wanalitunza ili liweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Alisema,kabla ya ujenzi wa daraja la mto Nyoka kulikuwa na daraja la muda lililojengwa kwa mbao na wakati wa masika lilikuwa linasombwa na maji hivyo kuleta ugumu wa huduma ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mbawala alisema,kujengwa kwa daraja katika mto Nyoka kumesaidia sana na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa vijiji vya wilaya ya Songea,Mbinga na nchi jirani ya Msumbiji ambao wanalitumia daraja hilo katika shughuli zao za kiuchumi.
MWISHO.
 

Vyombo vya moto vikipita katika daraja la mto Njoka linalounganisha kijiji cha Muhukulu-Kizuka-Mipeta hadi nchi jirani ya Msumbuji  lililojengwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Songea  ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao.
 

Mhandisi Davis Mbawala kushoto kutoka ofisi ya meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Songea,akikagua ubora wa kingo za daraja la mto Njoka linalounganisha kijiji cha Muhukulu-Kizuka na Mipeta wilayani Songea baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
 

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kizuka wanaoishi jirani na mto Njoka ambao hawakufahamika majina yao,wakimsikiliza kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Mhandisi Davis Mbawala aliyenyoosha mkono kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya daraja lililojengwa katika mto huo ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...