Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaongoza viongozi na wananchi katika kutoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu hayati Edward Ngoyai Lowassa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki pamoja na watanzania wote kwa ujumla kufuatia msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Makamu wa Rais amesema serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa aliyoutoa Hayati Edward Lowassa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa alijitolea kwa dhati kulitumikia Taifa pamoja na kutumia vema karama alizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika.

Amesema ni muhimu kila mmoja mtanzania kujikumbusha wajibu aliyonao kwa taifa na kuyaishi kwa vitendo mambo yote mazuri yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa.

Amesema ni vema Watanzania kumuenzi hayati Lowassa kwa kuendelea kuchapa kazi ili kuboresha maisha na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa kwa kuwa alikuwa mchapa kazi hodari katika utumishi wa umma na katika shughuli zake binafsi ikiwemo ufugaji.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote na hususan vijana kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwa manufaa ya Taifa kwa kuwa alikua kinara katika elimu na kusimamia kwa uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu hususan ujenzi wa shule za Sekondari kila Kata.

Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa mwanamazingira hodari ambapo katika wadhifa wake wa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Makamu wa Rais na alipokuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihimiza sana uhifadhi na Utunzaji wa mazingira.

Aliongoza kampeni nyingi za upandaji miti na usafi wa mazingira.

Amesema mchango wake huo uwakumbushe watanzania wote wajibu wa msingi wa kulinda na kutunza mazingira na hususan vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaendelea kuleta madhara mengi katika Taifa na dunia kwa ujumla.

Vilevile Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu akiwa msharika mzuri, akisali mara nyingi katika kanisa la KKKT Azania Front.

Amesema mfano huo ikumbushe kuwa kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na msingi wa mafanikio katika familia na katika utumishi wa umma.

Makamu wa Rais amewasihi watanzania kutumia msiba huo kudumisha na kuimarisha upendo, amani na mshikamano wa Taifa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa salamu za pole kwa familia, viongozi na wananchi kwa ujumla wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.





Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Regina Lowassa akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mume wake, Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa salamu za pole kwa familia wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.


Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa familia, wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akitoa pole kwa familia, wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitoa pole kwa familia, wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.









Baadhi ya viongozi na watu mashughuli wakiwa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam kwenye zoezi la kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoya tarehe 13 Februari 2024.


PICHA ZOTE NA OTHMAN MICHUZI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...