Na Mwandishi Wetu
 
KAULI ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kuweka wazi ukigeugeu wa Chama cha Chadema imezidi kuwaibua wadau wa siasa nchini wakiwemo wasomi ambo wamekitaka chama hicho kuwaomba radhi wananchi.

Wasomi na wachambuzi, wameshangaa kitendo cha CHADEMA kuendelea kuhamasisha maandamano na kukosoa baadhi mambo huku wakiacha kusema ukweli kwamba maridhiano hay ohayo yamewawezesha kupata ruzuku y ash. bilioni 2.7 ambayo waliigomea kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mwanasiasa mwenye historia kubwa ya siasa na uongozi nchini, Hamad Rashid Mohamed, aliipongeza CCM kwa miaka 47 ya kuzaliwa kwake chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. Samia ambaye ametembea ipasavyo mkakati wake wa 4R.

Alisema hatua ya Rais Dk. Samia kusimamia maridhiano na Bunge kupitisha miswada mitatu ukiwemo wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa yote ikiwa ya mwaka 2023 ni ya kupongezwa.

“Binafsi nimshukuru sana Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara mzee wetu Kinana kwa kweka wazi hili na huenda kuna mengi ya siri hatuyajui, hii ni aibu kwa viongozi wakuu wa chama hicho.

“Hii ni aibu na fedheha kwa Chama kikubwa cha upinzani kama CHADEMA kuwa na kauli mbilimbili, kauli za hadharani na sirini, huku kwa wananchi wakiwa wanajipambanua kuwa wao  ni chama cha ukweli na uwazi.

"Wamekuwa watu wa kuhimiza maandamano lengo lao ni kutafuta huruma za wananchi huku wakiwa wanapita mlango wa nyuma na kujichumia fedha kimya kimya,” amesisitiza

Amesema  kama kweli Chama hicho ni cha uwazi na uwajibikaji wakiri makosa yao na kuomba radhi kwa kuwa fedha hizo za ruzuku walizisusa kwa zaidi ya miaka mitatu wakiwa wametangaza hadharani, hivyo hatua ya viongozi kurudi kimya kimya na kuzichukua si jambo jema.

“Pia tutoe rai kwa hawa wenzetu waache kukitumia Kikosi kazi cha maridhiano vibaya na kujichumia matumbo yao, hawa watu wanachuma ndani ya serikali na wanachuma nje ya nchi kwa madai ya kuomba msaada katika kuimarisha demokrasia, hiki ndio kisebusebu sasa,” ameeleza.

Ameongeza  jambo hilo la kupokea zaidi ya sh. bilioni 2.7 lingekuwa jema kwao wasingefanya siri bali wangetangaza kama ambavyo wamekuwa wakitangaza mengine.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Doyo Doyo, alisema maridhiano yaliyonzishwa na Rais Dk. Samia yameleta umoja katika vyama vya upinzani huku akieleza awali ilikuwa huwezi kukaa ukumbi mmoja na wanachama wa CCM, lakini maridhiano yaliyoletwa na Rais Dk. Samia yameleta umoja kwa wanansiasa.
 
Wakati huo huo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Dk Thimothy Lyanga, amesema Kinana ametoa ufafanuzi namna Serikali ilivyofanikisha hatua ya maridhiano huku akihimiza siasa za kistaarabu.

Amefafanua  kutokana na kauli ya Kinana ni wazi CHADEMA wamefedheheka hivyo ni vyema kurudi na kuwa waungwana kwa kuuthibitishia umma kuwa ni kweli Rais Dk. Samia alikuwa mstaarabu na kuridhia wao kupata stahiki hizo za ruzuku.

“Uungwa ni CHADEMA kurudi na kuthibitisha katika uwanja wa siasa kuwa jambo hili ni kweli, uungwana unazaa amani na utulivu na wanatambua kuwa siasa zao zinachochea uvunjifu wa amani.

“Hiki ni chama kikubwa cha siasa wasipokuwa wakweli wawazi wanaendelea kupoteza sifa na heshima ambayo wananchi wanawapatia fedha hizi ni za umma wamechukua waseme,”alisema.

Amesema, hatua ya Rais kudhamiria kuwapo kwa maridhiano na kuongoza nchi kwa hekima na uvumilivu imelenga kuwapa nafasi wananchi ya kumchagua wamtakaye hivyo isitafsiriwe tofauti na vyama vya siasa kwa kulazimisha kuwapo na uongozi wa mabavu.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria(OUT) Dk. Mohamed Maguo amesema maridhiano ya kweli ndio yanayosababisha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.

Amesema Rais Dk. Samia amekuwa kiongozi wa mfano wa kulitaka taifa lisijigawe na ndio maana alizianzisha  4R kwa lengo la kutaka maridhiano ya kweli akianzia kwa wanasiasa.

“Nchi haiwezi kuwa na amani, utulivu,umoja na maendeleo bila ya kuwepo kwa maridhiano ya kweli na ndio maana tayari Rais Samia alishakaa meza moja na Mwenyekiti wa CHADEMA ili kutafuta suluhu ya kweli,”alisema Dk. Maguo.

Wakati huo huo mchambuzi wa masuala ya siasa nchini ambaye ni Mhadhiri wa  Chuo cha Mwalimu Nyerere Dk. Philip Daninga, amesema Rais Dk.Samia ana nia njema na watanzania na ndio sabbau ya kufanyia kazi yale ambayo yaliyokuwa yanaleta ugumu kwa wapinzani.

Ameongeza  Rais Dk. Samia alitumia 4R kwa kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani kwa lengo la kuleta haki katika vyama hivyo na si unyonge.

Pia amesema miaka 47 ya CCM Chama hicho kimeweza kupiga hatua hasa katika kutunza amani na utulivu vilivyopo nchini.

“Maridhiano ya kweli yanaleta amani ya kweli katika nchi na ndio maana Rais Dk. Samia tangu aingie madarakani anatafuta maridhiano ya kweli na vyama vya upinzani ili Taifa liongee lugha moja,”amesema.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...